Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhwani Jakaya Kikwete (Mb), amefungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, yanayofanyika kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026 yakibeba kaulimbiu isemayo, "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu."
Akizungumza Juni 17, 2026 wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo, Mhe. Ridhwani amesema maadhimisho hayo yanasaidia kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wananchi kwa kutoa fursa ya mawasiliano ya moja kwa moja kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi za umma.
Amesema maadhimisho hayo pia ni fursa kwa taasisi za umma kuonesha mafanikio, ubunifu na maboresho yaliyofanyika katika utoaji wa huduma, pamoja na kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidijitali ikiwemo e-Utendaji, e-Watumishi, e-Mrejesho, e-Ardhi, e-Office, GePG, MUVU, MAJIIS na TAUSI, ambayo imechangia kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za umma.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Kati wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bw. Novatus Mushi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, amesema ushiriki wa Baraza katika maadhimisho hayo unalenga kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira pamoja na kuwatambulisha huduma mbalimbali zinazotolewa na NEMC na mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma za mazingira.
"Tunatumia jukwaa hili kuelimisha wananchi kuhusu wajibu wao katika kulinda mazingira na kuwafahamisha huduma mbalimbali zinazotolewa na NEMC pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali kama e-Mrejesho, e-Office na Mazingira App ili kupata huduma kwa urahisi zaidi," amesema Bw. Mushi.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu yamezikutanisha zaidi ya taasisi 200 za umma na wadau mbalimbali katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.



















EmoticonEmoticon