TANZANIA YAPIGA HATUA KATIKA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA UKIMWI

November 14, 2024



Na. Aron Msigwa – MAELEZO.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderianaga ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya UKIMWI kufuatia kupungua maambukizi ya Virusi Vvya Ukimwi (VVU) na idadi ya watu wanaoishi na virusi hivyo nchini kutoka 1,700,000 mwaka 2017 hadi kufikia 1,540,000 mwaka 2023 huku akiyataja baadhi ya makundi yakiwemo ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, madereva wa masafa marefu, wachimbaji wadogo wa madini na wavuvi kuchangia maambukizi mapya ya ugonjwa huo hapa nchini.


Mhe. Ummy ameyasema hayo leo (Novemba 14, 2024) jijini Dodoma alipokua akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani kwa mwaka 2024 ambayo kitaifa yatafanyika Desemba 1, 2024 mkoani Ruvuma yakiongozwa na kaulimbiu isemayo Chagua Njia Sahihi, Tokomeza Ukimwi inayolenga kutokomeza ugonjwa huo kama janga la kiafya kufikia maambukizi sifuri ifikapo mwaka 2030.



“Mafanikio tuliyoyapata kwenye mwitikio wa mapambano dhidi ya Ukimwi yamechangiwa na nchi yetu kulinda na kuheshimu haki za binadamu na raia ikiwa ni pamoja na haki ya kupata huduma za afya na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, uwekezaji kwenye sekta ya afya ya jamii kupitia ujenzi wa miundombinu ya hospitali, vituo vya afya na zahanati na uimarishaji wa mifumo ya utoaji wa huduma za kinga dhidi ya VVU, tiba na matunzo” amesisitiza Mhe. Ummy.


Ameongeza kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu atakua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na yataambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za wadau, mdahalo wa vijana na viongozi wa kidini na kimila, kongamano la kitaifa la kisayansi kwa ajili ya kujadili mada mbalimbali kuhusu mwitikio wa Taifa kuhusu Ukimwi, utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za ushauri  na upimaji wa hiari wa VVU na utoaji wa elimu kuhusiana na VVU. 



“Watanzania tutaungana pamoja kufanya maadhimisho haya kwa lengo la kutafakari, kutathimini na kuangalia juhudi tunazozifanya katika mapambano dhidi ya VVU sambamba na kuthamini juhudi za wadau mbalimbali katika kupambana na UKIMWI” ameeleza Mhe. Ummy.


Aidha, amesema kupitia Ofisi ya Rais -TAMISEMI mikoa yote nchini imeelekezwa kuandaa na kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani kwa Wakuu wa Mikoa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU na Ukimwi kuhamasisha wananchi katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na familia, sehemu za kazi, nyumba za ibada, shule na vyuo kushiriki maadhimisho haya kwenye maeneo yao.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dkt. Jerome Kamwela amesema kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu TACAIDS ina jukumu la kuwaleta wadau wote wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya VVU kuonesha shughuli wanazofanya na huduma wanazotoa ili kuendeleza mapambano hayo.


“Maadhimisho ya mwaka huu yatashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za afya, taasisi za kidini na makundi mbalimbali ya uelimishaji ambapo kuanzia Novemba 22, 2024 tutaanza kutoa huduma zetu katika maeneo mbalimbali tukiwa mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuandaa kilele cha maadhimisho hayo" Amesema Dkt. Jerome.


Amesema TACAIDS imeweka mikakati ya kupunguza maambukizi ya VVU kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ambalo ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi mapya hapa nchini kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelimishaji kupitia vituo vya malori ya masafa marefu katika barabara kuu kuanzia Dar es salaam kuelekea mikoa Morogoro, Dodoma, Tabora, Mwanza mpaka Mbeya mpaka Tunduma.


Kuhusu hali ya maambukizi ya Ukimwi nchini amesema yameendelea kupungua akitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya na kuchagua njia sahihi katika kupambana na ugonjwa huo kwa kujielimisha, kuepuka tabia hatarishi, kutumia dawa na njia sahihi kwa wale wanaoishi na VVU.


Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la UNAIDS Tanzania, Dkt. Martin Odit  ameeleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayofanyika kila mwaka ni njia pekee ya kuikumbusha jamii kuendelea kupambana na kutokomeza ugonjwa huu huku akisistiza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuchagua njia sahihi za kutokomeza VVU na kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na UKIMWI, unyanyapaa na ukosefu wa huduma muhimu.


“Naishukuru Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya dhidi ya VVU hali inayotoa mwanga katika kuhakikisha tunafikia maambukizi Sifuri mwaka 2030.


Mwakilishi wa Baraza la Watu Watu Wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA), Emmanuel Msinga ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yenye kauli mbiu isemayo Chagua Njia Sahihi, Tokomeza Ukimwi yanatoa fursa ya kuwezesha kupanga malengo ya kupunguza unyanyapaa, kupunguza maambukizi mapya na ubaguzi kufikia sifuri ifikapo 2030.

Amesema katika maadhimisho hayo mkoani Ruvuma wao kama Baraza watatoa elimu kuhusu VVU na kuendesha shughuli za upimaji pamoja na kuwaambia Watanzania kuwa kuishi na VVU sio mwisho wa maisha. 


" Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kuwa watu tunaoishi na VVU tunapata huduma zote muhimu jambo ambalo linatufanya tuishi vizuri na kuwa na afya nzuri kama sawa sawa na wenzetu ambao hawana VVU pamoja na uwezeshaji kiuchumi katika shughuli za maendeleo”

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »