Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wazazi na walimu kushirikiana kuwaandaa wanafunzi wao kuwa viongozi na wazazi bora kwa siku zijazo.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septema 30, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Elimu iliyofanyika Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga iliyobeba kaulimbiu "Mtoto wa leo, Samia wa kesho" ambayo inalenga kuboresha ufaulu katika wilaya hiyo na mkoa wa ujumla.
“ Wazazi, walimu na wanafunzi ni falsafa ya utatu unaoweza kutengeneza wazazi na viongozi wazuri na bora kwa siku za baadaye, ‘’amesema Dkt. Biteko.
Amefafanua “ Mwalimu, mtoto anayekuja mbele yake amuone kama injinia, daktari, mbunge, Rais wa kesho, kiongozi na mzazi bora wa kesho na sio mteja anayepata huduma na kuondoka zake.”
Pia, Dkt. Biteko amewataka wazazi kuwa na kiu ya watoto wao wa leo kuwa Samia wa kesho kwa kushirikiana na walimu kutengeneza viongozi na wazazi bora wa baadaye kwa kuwajengea misingi ya kujiamini na hatimaye kutimiza ndoto ya kuwa viongozi bora.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia imewekeza katika sekta ya elimu ili kupata matokeo na maendeleo yanayoendana na uwekezaji huo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Zainab Katimba amesema kuwa Serikali imejipanga kuwaandaa viongozi bora wa kesho kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu na miundombinu mbalimbali ili kuandaa mazingira bora ya kujifunzia.
Akizungumzia sekta ya afya Mhe. Katimba amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kupandisha hadhi Zahanati ya Mgambo kuwa Kituo cha Afya kuanzia mwaka huu wa fedha ambapo zaidi ya shilingi milioni 649 zimetengwa kwa ajili ya uboreshaji wa kituo hicho.
Vilevile, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga amesema kuwa Wizara yake itaendelea kuandaa sera na miongozo mbalimbali inayojikita katika maendeleo ya elimu nchini.
Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mwana FA) ameishukuru Serikali kwa kuboresha mazingira na miundombinu ya elimu wilayani Muheza na kuongeza kuwa Wilaya hiyo ina mahitaji ya shule amali.
Aidha, Mhe. Mwinjuma kwa kushirikiana na marafiki zake wamejenga shule ambayo inatarajiwa kuanza kutoa huduma mwaka 2025 ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amemshukuru Rais Samia kwa kuupatia mkoa wake fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya umeme, barabara na elimu inayolenga kusaidia wananchi kupata huduma bora.
Aidha, Dkt. Burian ametumia amewasisitiza wakazi wa Mkoa wa Tanga kujiandikisha na kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na baadaye kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Awali, DKt. Biteko alikagua maonesho shughuli mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono Wiki ya Elimu Wilayani Muheza
EmoticonEmoticon