Ashrack Miraji,Same
Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameagiza Serikali ya Kata ya Kirangare kushirikiana na Wakazi wa Kijiji cha Kirangare na Makasa kumaliza simtofahamu iliyopo ya mgogoro wa mipaka ya vijiji hivyo viwili licha ya idara ya ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Same kutatua mgogoro huo hapo awali kwa kubainisha mipaka hiyo kwa mujibu wa ramani.
Kwa mujibu wake Afisa ardhi mteule Halmashauri ya Wilaya ya Same Sampa Angelina alisema ..“Tulifanya kikao cha kwanza tukakubaliana Serikali zote mbili tukutate, mara ya pili tulipokuja kukutana na Serikali mbili upande wa Kirangare hawakutaka kwenda kwenye mipaka, kwahiyo mwisho wa siku wajibu wetu kama Ofisi ya ardhi ilikuwa ni kuonesha mpaka kwa mujibu wa ramani na ndicho kilichofanyika”. Alisema Afisa ardhi wakati akitolea ufafanuzi wa mgogoro huo kwenye mkutano wa hadhara.
Aidha baadhi ya wazee kwenye mkutano huo walitoa maoni yao juu ya mgogoro huo ambapo walisema njia moja wapo ya kumaliza simtofahamu hiyo ni kukutanisha wazee wa pande zote mbili ambao ndiyo wanafahamu kwa undani mipaka ya vijiji hivyo, itumike busara na baada ya hapo vijana wao watii maamuzi yatakayotolewa baada ya pande zote mbili kukubaliana uhalali wa mipaka hiyo.
Hata hivyo hali hiyo imemlazimu Mkuu huyo wa Wilaya kuelekeza Serikali ya Kata ya Kirangare kusimamia kwa karibu kumaliza simtofahamu hiyo kwa kutumia hekima na busara kuzikutanisha pande hizo mbili kubaini sababu inayopelekea kuwepo kwa mgogoro licha ya suluhu kupatikana kwa mujibu wa sheria za ardhi.
“Wale wa Makasa ni ndugu zenu walitoka Kirangare, kaeni pamoja mpitie pamoja kama kuna marekebisho kwa pamoja mzungumze kumaliza mgogoro kwa upendo nyinyi ni ndugu”. Alise DC Kasilda.
Kijiji cha Kirangare na Makasa awali kilikuwa kijiji kimoja, mgogoro huo umeibuka baada ya kugawanywa kwa maeneo ya utawala na kuwa vijiji viwili kati ya vitatu vinavyo unda Kata ya Kirangare, ambavyo ni Kirangare, Makasa na Hedaru.
Pamoja na maelekezo hayo aliyotoa lakini pia DC Kasilda alihimiza wananchi kushiriki zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha kwenye daftari la mkazi linalofanyika kwa muda wa siku kumi kuanzia Oktoba 11 hadi 20 ili waweze kuchagua viongozi bora na wenye uchungu na wananchi wao ifikapo Novemba 27 mwaka huu 2024.
EmoticonEmoticon