WAZIRI UMMY AMUAGA BALOZI WA SWITZERLAND

July 30, 2024

 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa shukrani kwa nchi ya Switzerland kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia Sekta ya Afya hasa kwenye uboreshaji wa Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi nchini. 

Waziri Ummy amesema hayo leo Julai 29, 2024 wakati akiagana na Balozi wa 'Switzerland' nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot katika ofisi ndozo za Wizara ya Afya Jijini Dar Es Salaam aliyedumu kwa muda wa Miaka Minne nchini. 

"Tanzania na Uswisi zina ushirikiano wa muda mrefu wa maendeleo kupitia Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC), maeneo ya sasa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi ni pamoja na kuendelea kuchangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja ambapo kupitia awamu ya ufadhili wa moja kwa moja wa Kituo cha Afya (DHFF) Mwaka 2021-2025." Amesema Waziri Ummy 

Waziri Ummy amesema nyanja nyingine wanayoshirikiana na Uswisi ni katika kuchangia kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030, mpango wa kulinda Afya za vijana (SYP) pamoja na kutoa msaada kwa nafasi ya usimamizi wa ubia na uhamasishaji wa rasilimali ili kusaidia Wizara ya Afya. 

Waziri Ummy ameiomba Serikali ya Uswisi kuiunga mkono na kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuendelea kuchangia Mfuko wa Afya wa pamoja na kusaidia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili Watanzania wapate huduma za Afya bila kikwazo cha fedha. 

Kwa upande wake Balozi wa Switzarland Mhe. Didier Chassot ameihakikishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kushikiana hasa katika upande wa Sekta ya Afya ikiwemo kuchangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja. "Nitaenda kumweleza mwenzangu anaekuja baada yangu jinsi tulivyokuwa tunashirikiana na Serikalinya Tanzania hasa katika kuchangia Mfuko wa Afya wa pamoja lakini pia na ombi hilo la kusaidia kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote." Amesema Balozi Chassot

Balozi Chassot ameishukuru Tanzania kwa kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ambapo pia ameelezea jinsi Watanzania walivyo wakarimu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »