WAZIRI MBARAWA AITAKA TANROADS KUSIMAMIA JENGO LA ABIRIA TABORA

January 30, 2024

 

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora, jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo na kuhudumia abiria takribani 120 kwa wakati mmoja.
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi, Dkt. Batlida Burian, wakati Waziri huyo alipomtembelea Mkuu wa Mkoa huyo ofisini kwake Mkoani Tabora.
PICHA NA WIZARA YA UCHUKUZI

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha mradi wa Jengo la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Tabora unaotekelezwa na Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Beijing Construction Enginerring Group CO. Ltd unakamilika ndani ya muda atakaoongezwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Mkoani humo Waziri Prof. Mbarawa amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza tayari Serikali imechukua hatua stahiki ili kuhakikisha mradi huo unakamilishwa ili kuiunganisha Tabora na mikoa mingine kwa njia ya usafiri wa anga..

“Mradi huu ulisainiwa muda mrefu lakini utekelezaji wake umeanza mwaka jana na hiyo ilitokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza hivyo TANROADS msimamieni kwa karibu Mkandarasi huyu ili akamilishe ndani ya muda atakaoongezewa ili kuchagiza usafiri wa anga na kukuza uchumi wa mkoa’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ameipongeza TANROADS kwa kuhakikisha wazawa wanapewa kipaumbele katika ajira hali inayowafanya wananchi kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huku wakinufaika kwa kupata kipato.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi, Dkt. Batlida Burian, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuzingatia na kuhakikisha Tabora inakuwa kitovu cha Usafiri na Usafirishaji kwani kupitia mradi wa Kiwanja cha ndege na reli ya Kisasa ya SGR utachochea shuguli za maendeleo na uchumi mkoani humo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa changamoto zitokazokubaliwa ili kuruhusu kuongeza muda kwenye mradi utazingatia uhalisia ili kuukamilisha kwa viwango na thamani ya fedha.

Aidha, Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora Fadhili John amesema kukamilika kwa jengo hilo kutawawezesha abiria takribani 120 kuhudumiwa kwa wakati mmoja.



Mradi wa Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora unaotekelezwa na Kampuni ya M/S Beijing Construction Enginerrging Group Co. Ltd ambao kwa sasa umefikia asimilia 27 unagharimu takribani shilingi bilioni 24 ambapo pamoja na jengo hilo ujenzi huo unahusisha ujenzi na ufungaji wa mnara wa kuongozea ndege, barabara za kuingia na kutoka Kiwanjani, uzio pamoja na kontena la hali ya hewa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »