CRDB YAPANDA MITI 500 SIMANJIRO

January 19, 2024



Na Mwandishi wetu, Simanjiro



BENKI ya CRDB katika kuadhimisha wiki ya jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania, imepanda miti 500 Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa lengo la kutunza mazingira na kurejesha uoto wa asili.


Mwenyekiti wa jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania, sheikh Alhad Mussa Salum amefanya uzinduzi huo wa kitaifa kwa kupanda miti kwenye zahanati ya kijiji cha Nakweni, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara.


Sheikh Alhad ambaye pia ni balozi wa kampeni ya mazingira kwenye ofisi ya Makamu wa Rais amesema uzinduzi huo ni wa kitaifa na kilele chake kitafanyika Machi 6 mwaka 2024 jijini Mbeya.


Sheikh Alhad amewapongeza CRDB kwa kutoa miche hiyo 500 ambayo itakuwa imetunza mazingira ya eneo hilo la Nakweni na kuwanufaisha watu wanaozunguka eneo hilo.


Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera, amewataka wakazi wa kijiji cha Nakweni kuitunza miti hiyo kwa kutoachia mifugo kuzagaa na kuiharibu.


"Hili ni tukio la kitaifa kwa kukusanya viongozi wakubwa kuja kupanda miti hivyo tujitahidi kuitunza miti hii na kuwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye, kwa kunufaika na kivuli na matunda," amesema DC Serera.


Meneja wa CRDB, kanda ya kaskazini, Cosmas Sadat amesema wameungana na jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania kwa kuadhimisha siku hiyo ndiyo sabuni wakatoa miche 500 ili kuwaunga mkono.


"Benki ya CRDB ni mdau mkubwa wa maendeleo mbalimbali nchini katika sekta ya elimu, afya, mazingira na mengine, ndiyo maana tukachangia miche hiyo 500 ya matunda na vivuli ambayo itakuwa manufaa ya wakazi wa Nakweni kata ya Shambarai," amesema Sadat.


Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, amewashukuru jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania kwa kuadhimisha siku hiyo wilayani Simanjiro kwani wamewapa heshima kubwa mno.


"Tunawashukuru mno CRDB kwa kutoa miti hiyo 500 nasi tunaahidi kuitunza na kuongeza miche mingine kwa lengo la kuwashukuru na kuwaunga mkono kwenye jambo hili la kitaifa," amesema Ole Sendeka.


Diwani wa kata ya Shambarai, Julius Lendauwo Mamasita, amesema upandaji wa miti hiyo kwenye zahanati hiyo utawanufaisha jamii ya eneo hilo hasa wanawake wajawazito kwani watapata eneo zuri la kupumzikia.


"Jamii ilikuwa inatembea umbali mrefu wa kilomita 35 hadi mji mdogo wa Mirerani kufuata huduma za afya, tunawashukuru CRDB kwa kutoa miti hiyo ambayo itakuwa faida kwetu miaka ijayo," amesema Mamasita.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »