Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WANAFUNZI 49 wa Shule ya Mikocheni Islamic wamehitimu elimu ya msingi (darasa saba) huku uongozi wa shule hiyo ukijivunia elimu wanayoitoa ambayo inawajenga watoto kuwa raia wema kwa taifa la Tanzania sambamba na kuwajengea nidhamu na heshima.
Wakati mgeni rasmi katika mahafali hayo ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Abdi Mkeyenge akitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa jamii kuhakikisha wanakuwa wasisimizi wa watoto katika kutumia teknolojia katika kujenga na si kuharibu.
Akizungumza wakati wa mafahali ya wanafunzi wa shule hiyo ambao wamehitimu elimu ya msingi kwa maana ya darasa la saba Mkeyenge amesema kwa sasa kumekuwa na matumizi makubwa ya teknolojia lakini ni vema kwa watoto ikatumika vizuri.
“Teknolojia si mbaya kwa maana ya asilimia 100 lakini ina uzuri na ubaya wake sasa inategemea wewe utatumia ili ikuletee faida au hasara.Kwa maana ya faida ni kweli tutumie teknolojia ituzalishie.
“Kwa mfano siku hizi unaweza kuipata dunia yote ukiwa kwenye simu yako kiganja chako kwa hiyo inategemea unatumia kwa ajili ya nini lakini kwa watoto nimesisitiza wazazi na walezi tutumie teknolojia iwafae watoto sio.
“Kwa maana umuachie anakuwa huru kutumia kifaa ambacho kina teknolojia na yeye mwenyewe akajiamualia afanye nini, unaweza kumuachia akatumia lakini kifaa kiwe na udhibiti na awe na mipaka ya kutumia hicho kifaa anapokuwa nyumbani, kama luninga uweke mambo ambayo yanaendana na umri wake kama ni simu awe anatumia katika masomo,”amesema.
Kuhusu malezi ameipongeza shule hiyo kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwalea watoto wa kimisingi ya kimaadili yakiwemo ya dini , hivyo amewataka walimu kuendelea na kusimamia maadili lakini na wanafunzi nao kujivunia utamaduni wa shule hiyo na wajivunie walivyo kokote watakakokwenda.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mikocheni Islamic Zuwena Hamis amesema jumla ya wanafunzi 49 wamehitimu elimu ya msingi wakiwemo wasichana wakiwa 29 na wavulana 20 huku akieleza namna wanavyojivunia kutoa wanafunzi walioiva katika masomo ya elimu ya kimazingira na vitendo.
“Tunajivunia msingi imara wa wanafunzi ambao tunategemea watakuwa mabalozi wetu na raia wema kwasababu tumewafundisha maadili kwa vitendo, wameiva kimazingira lakini katika maadili.
“Tumetoa wanafunzi ambao wako vizuri katika sayansi, wako vizuri katika vitendo, wako vizuri katika heshima na nidhamu lakini wameiva katika eneo la imani dini.”
Amefafanua kwa sasa ulimwengu umebadilika hivyo mwanafunzi anahitaji kulelewa katika mazingira yote ikiwemo kupewa elimu ya mazingira, elimu ya vitendo na anahitaji kupewa maadili na malezi mema yanayomuwezesha kumsaidia kuwa raia bora na kijana bora wa hapo baadae
“Kwa hiyo hili ni jambo kubwa tunalojivunia kwamba elimu tunayotoa ni kwa njia ya vitendo, tukimfundisha dini tunafundisha kwa vitendo, kama heshima tunafundisha kwa vitendo na kama ibada tunafundisha kwa vitendo.Watoto wetu wameiva katika maeneo yote.”
Akitoa ujumbe kwa wazazi na walezi, amesema ni vema wakatambua wanapowafundisha wanafunzi wanafundisha vitu ambavyo viko katika mpangalio lakini wanapofika nyumbani wazazi wamekuwa na majukumu mengi hivyo hawapati nafasi ya kusimamiwa nyumbani.
“Watoto wanatumia muda mwingi kuangalia luninga na mitandao mingine ya kijamii ambayo hawaitumii kwa usahihi.Wanakuwa wanapoteza muda mwingi kwa mambo yasiyokuwa na faida lakini wazazi hawajui kwa kuwa wanatoa nyumbani mapema na kurudi usiku.”
Aidha amesema kumekuwa na changamoto ya mtoto kulelewa na mzazi mmoja aidha baba au mama na hilo ni tatizo kubwa linaloathiri watoto , hivyo ameshauri wazazi kuangalia hatma ya watoto wao kwa kuhakikisha wanavumiliana na wanaishi pamoja.
“Wazazi hawafikirii kwamba ndoa ni kitu cha msingi ambacho baba na mama wakiwa pamoja malezi ya watoto yanakuwa mazuri .Wanapokuwa mbalimbali watoto wanaathirika kwa kiwango kikubwa,wanachanganyikiwa kimasomo na wanakosa mapenzi ya wazazi wote wawili, hivyo ni vema wazazi wakakubaliana ili kutengeneza familia iliyo bora.”
Wahitimu wa Shule ya Mikocheni Islamic wakitumbuiza wakati wa mahafali hayo
Mwanafunzi Sakina Rashid akisoma rasala yao mbele ya mgeni rasmi na wageni waalikwa wakati wa mahafali hayo .
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania( TASAC) Abdi Mkeyenge akizungumza wakati wa mahafali hayo ya shule ya Mikocheni Islamic iliyopo jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa bodi ya Wadhamini Shule ya Mikocheni Islamic Alhaj Othman Janguo akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi wakati wa mahafali hayo
Mwalim Mkuu wa Shule ya Mikocheni Islamic Zuwena Hamis akizungumza wakati wa mahafali ya darasa la saba la wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2023
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Mikocheni Islamic
EmoticonEmoticon