NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, DAR ES SALAAM.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amefungua semina elekezi kwa Wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) jijini Dar es Salaam Septemba 11, 2023.
Akizungumza na wastaafu hao kutoka mkoa wa Dar es Salaam, Profesa Ndalichako aliipongeza PSSSF kwa kuandaa semina hiyo iliyobeba kauli mbiu isemayo “Wekeza Mafao yako Sehemu Salama kwa Uhakika wa Ukwasi”.
Alisema lengo la semina hiyo ni kuwajengea wastaafu wake watarajiwa uelewa na ufahamu juu ya umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi ya kukuza vipato vyao baada ya kustaafu ili kuleta tija na uendelevu wa kipato.
“Usia wangu kwenu ni kuyatumia vyema madini ya elimu mtakayoyapata hapa kwa kushikilia mambo makuu matatu nayo ni kuwa na mtazamo chanya, kuweka mipango makini na kutimiza ndoto binafsi baada ya kustaafu.” Alisema Profesa Ndalichako.
Alisema kustaafu ni wajibu kwa kila mtumishi hivyo hakuna budi kuendeleza maisha mazuri hata baada ya kustaafu.
Alisema ni vema mtumishi akatambua kuwa safari ya kustaafu inaanza pale anapoanza ajira, hivyo ni muhimu kujiandaa kimipango na kifedha ili kufurahia maisha ya uhuru lakini umakini katika usimamizi wa fedha.
“Matumizi ya busara ya fedha baada kustaafu ni muhimu zaidi kwani kwa kiasi kipato kinapungua na nguvu za kufanya kazi zinaenda zikipungua siku hadi siku,” aliasa.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema PSSSF inatarajia kuwa na wastaafu 11,000 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema Wastaafu watapatiwa mafunzo ya elimu ya uwekezaji katika masoko ya fedha, taarifa za nyaraka na utaratibu wa kufuata wakati wa kustaafu, kujiandaa kisakolojia baada ya kutoka kwenye utumishi, umuhimu wa kutunza mazingira tunayoishi kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, na uhalifu wa kimtandao ambao unawaathiri wastaafu wengi.
“Mfuko katika kutambua na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, una mpango wa kutoa mche mmoja wa mti kwa kila mstaafu wa PSSSF.
“Mpaka sasa tuna wanachama 739,000 na lengo hapa ni kila mmoja aweze kupanda na kuutunza mche tutakaompatia pindi atakapofikia wakati w akustaafu.”Alifafanua CPA. Kashimba.
Semina kama hii ilifanyika mwaka 2021 kwa wastaafu watarijiwa 3700 bara na visiwani na mwaka huu pia elimu itawafikia wastaafu kwenye mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani, alisema CPA. Kashimba.
CPA. Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mkuu, PSSSF, akizungumza na wastaafu watarajiwa
Baadhi ya washiriki wa semina wakifuatilia hotuba ya mhgeni rasmi.
Baadhi ya watendaji wa Mfuko.
EmoticonEmoticon