WAZIRI MAVUNDE ATOA MWELEKEO MPYA SEKTA YA MADINI

September 11, 2023


Aainisha dira ya “madini ni maisha na utajiri ya mwaka 2030”_ 


 _Wizara kuwekeza nguvu kwenye utafiti wa madini_ 

 *DODOMA* 

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa shughuli za utafiti wa madini nchini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kutoa taarifa sahihi za kijiolojia za madini na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi sambamba na kuwawezesha wachimbaji wadogo.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Septemba 11, 2023 kwenye kikao chake na uongozi wa Tume ya Madini kupitia ziara yake aliyoifanya kwenye Ofisi za Tume Makao Makuu jijini Dodoma yenye lengo la kupokea taarifa za majukumu ya Tume, kubaini changamoto na kuzitatua.

Amesema kuwa, ili kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Madini, Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeweka mkakati wa kuhakikisha tafiti za kijiolojia zinafanyika katika maeneo yote nchini ifikapo mwaka 2030 ili kuwezesha wachimbaji wa madini wengi kuendesha shughuli zao bila kubahatisha na Serikali kuendelea kupata mapato ambayo yatawezesha kuimarisha sekta nyingine muhimu kama vile miundombinu, kilimo, nishati n.k.

“ Tafiti hizi  zitawezesha kugundulika kwa madini ya kimkakati, malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea hali itakayopelekea uwepo wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini, kuzalisha ajira mpya katika Sekta ya Madini na sekta nyingine na kupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini na wachimbaji wakubwa wa madini,” amesema Mavunde.

Katika hatua nyingine, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipokuwa Waziri wa Madini na kuongeza kuwa ataendeleza kazi nzuri iliyofanywa sambamba na kuomba ushirikiano kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini ili kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unafikiwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 huku wananchi wakiendelea kutajirika kutokana na uwekezaji katika Sekta ya Madini.

Aidha, amepongeza kasi ya Tume ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa kwenye ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli kila mwaka, uanzishwaji wa masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini nchini 95, kuimarika kwa usimamizi wa usalama wa afya na mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuitaka Tume kuongeza ubunifu kwenye utendaji kazi.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akizungumza kwenye kikao hicho sambamba na kupongeza kwa uteuzi wa Waziri Mavunde amesema kuwa Wizara na Taasisi zake ipo tayari kumpa ushirikiano ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa miongoni mwa sekta zinazoongoza mchango wake katika  ukuaji wa uchumi wa nchi.

Awali akieleza mafanikio ya Tume ya Madini tangu kuanzishwa kwake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa  ni pamoja na ongezeko la makusanyo ya maduhuli kutoka shilingi bilioni 346.27 mwaka 2018/2019 hadi shilingi bilioni 678.04 mwaka 2022/2023 na utoaji wa leseni za madini 36,157 zikiwemo leseni za utafutaji wa madini 984, leseni za uchimbaji wa kati wa madini 89, leseni za uchimbaji mkubwa wa madini nne, leseni za uchimbaji mdogo wa madini 21,707 na  leseni za uchenjuaji wa madini 174.

Ameongeza kuwa leseni za madini nyingine ni pamoja na leseni za usafishaji wa madini nane, leseni za uyeyushaji wa madini sita, leseni ndogo za biashara ya madini 9,851 na leseni kubwa za biashara ya madini 3,335.

Mhandisi Lwamo ameongeza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ambapo katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Tume ilifanya kaguzi kwenye migodi midogo 32,400 katika mikoa yote 30 ya kimadini nchini pamoja na kuimarika kwa udhibiti wa utoroshaji wa madini nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »