TAWA YAPEWA TUZO NA OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE NA URATIBU

September 12, 2023

 

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imeipatia Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) tuzo maalum kwa ajili ya kutambua na kuthamini mchango wake katika kufanikisha Kongamano la Pili la wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.

Tuzo hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko wakati akifungua kongamano hilo ambapo ameipongeza TAWA huku akiwasilisha salamu za Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa za kuwasihi na kuwapongeza washiriki kwa kuweka ratiba ya kutembelea hifadhi za taifa, mapori tengefu na vivutio vingine vya utalii vilivyopo ukanda wa kaskazini mwa Tanzania.

“Mhe. Waziri Mkuu amenituma niwaambie amefurahi sana kusikia kuwa kwa mujibu wa ratiba yenu mtakwenda kutembelea vivutio vya utalii hivyo amewasihi sana mkirudi mlikotoka mkawe mabalozi wema kwa nchi yetu na kutangaza vyema Tanzania”

Kando na hilo, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amewataka maafisa masuhuli wote nchini kuviwezesha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara na taasisi zao kwa kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wa kutosha, vitendea kazi na rasilimali fedha ili viweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.



Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulika na masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema, wakati kongamano hili likifanyika kwa mara ya Pili hapa nchini, Serikali imefanyia kazi kwa Asilimia mia, (100%) utekelezwaji wa agizo la uanzishwaji wa Idara za Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara na Serikali.

Awali akiongea wakati wa Ufunguzi wa Kongamano hilo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, alisema kwa kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa kujipima matokeo, Taasisi za Umma zinaweza kujihakikishia kuwa zipo katika njia sahihi za utekelezaji katika kufikia malengo yake, hivyo Ufuatiliaji na Tathmini ni njia nzuri ya kujifunza na kuwajibika.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »