TUNATAKA KUWA NA MIFUMO MICHACHE YA TAARIFA ZA AFYA INAYOWASILIANA; DKT. SHEKALAGHE

August 15, 2023

 

Na WAF, Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amewataka wataalam wa TEHAMA kufanyia kazi mifumo ya taarifa ya Wizara ili iweze kuwasiliana na kuwa na mifumo michache yenye kuleta tija na kurahisisha utoaji wa huduma.

Dkt. Shekalaghe amesema hayo alipokuwa akifungua kituo cha umahiri katika masuala ya afya kidigitali Jijini Dodoma.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza kuanza kwa matumizi ya tiba mtandao lakini pia ameelekeza kwamba lazima mifumo yetu ipungue, ninafurahi siku ya leo ni moja ya hatua ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais. Wataalam wetu wakikaa hapa wataweza kuja na suluhisho la changamoto za mifumo iliyopo na kuwa na mifumo michache yenye tija” amesema Dkt. Shekalaghe


Amesema, kituo hicho cha umahiri katika masuala ya kidigitali (CDH) kitasaidia kuunganisha mifumo ya Sekta ya Afya pamoja na kupunguza mifumo iliyopo katika Wizara ya Afya.

“Kituo hiki kitasaidia kupungua kwa mifumo mingi ambayo haitazidi mifumo Minne au Mitano lakini pia kuwezesha kuunganisha mifumo iliyopo kwa kuweza kusomana ndani ya Wizara ya Afya”, amesema Dkt. Shekalaghe

Vile vile, Dkt. Shekalaghe amesema kuwa taarifa zinazotolewa na kituo hicho ziweze kutumika kwa ajili ya tafiti zitakazotuwezesha kufanya maamuzi mazuri zaidi.

“Tunataka kuwa na taarifa zote kamilifu na muhimu zinazosaidia utoaji wa huduma za matibabu, mtu ukifika hospitalini taarifa zako kuanzia mapokezi, vipimo na matibabu ziweze kuingizwa na kutunzwa kwenye mifumo yetu hii na iweze kuzungumza na kwa kuanzia tayari tunayo AFYA CARE, ambayo ipo tayari kwenye hospitali ngazi ya Mikoa kwenda juu, na GOTHOMIS ambayo inatumika kweney vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi” amesema Dkt. Shekalaghe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la PATH Bw. Amos Mugisha amesema wamewezesha kukarabati wa kituo hicho, kuweka samani pamoja na vifaa vya kiteknolojia.

Amesema, moja ya umuhimu wa kituo hicho ni kuweza kutengeneza mifumo ambayo inazungumza na kupunguza mifumo mingi iliyopo katika Sekta ya Afya kwa sasa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA Wizara ya Afya Bw. Silvanus Ilomo amesema kuwa kituo hicho kitatumiwa siyo tu na Wizara ya Afya bali wataalam wengine wa Sekta ya Afya kwa ajili ya kukutana na kuja na mifumo yenye tija katika uboreshaji wa huduma za afya nchini.

“Kituo hiki ni mali ya Serikali, wataalam wote wa Sekta mnakaribishwa kuja kufanya kazi hapa kwa kuwa hii ni Serikali moja na haya ni mafanikio ya Serikali hii”, amesema Bw. Ilimo.    


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »