Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akipata ufafanuzi toka kwa mhandisi mkazi anayesimamia ujenzi wa barabara ya Tungumaa-Mkwaja-Mkange KM 95.4 alipokagua ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha wilaya za Handeni, Bagamoyo na Pangani mkoani Tanga.
Muonekano wa moja ya daraja katika barabara ya Tungumaa-Mkwaja-Mkange KM 95.4 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa mkandarasi M/s Shandong Luqiao Group Ltd anayejenga daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na barabara za maingilio takriban KM 25 mjini Pangani
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mbunge wa Pangani ambaye pia ni waziri wa maji mhe. Jumaa Aweso alipokagua ujenzi wa daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525.
Muonekano wa baranbara ya Tanga–Pangani KM 50 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewataka wakandarasi wanaojenga barabara za Tanga-Pangani KM 50, Tungumaa-Mkwaja-Mkange KM 95.4 na daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 mkoani Tanga kuongeza wataalam na mitambo ili kuharakisha kazi za ujenzi huo.
Prof. Mbarawa amesema Serikali haitasita kuchukua hatua za kimkataba kwa mkandarasi yeyote anayeshindwa kuajiri wataalam sahihi na wakutosha na hivyo kusababisha miradi kuchelewa kumalizika na kuwanyima wananchi fursa ya kunufaika na miradi hiyo mapema.
“Tunaleta fedha na tutaendelea kuleta kwa awamu hivyo hakikisheni wataalam stahiki wapo site na mitambo ifike kwa wakati ili kulinda dhana ya value for money”, amesema Prof. Mbarawa.
Amewataka wakandarasi M/s China Henan International Cooperation Group Co. Ltd anayejenga barabara ya Tanga-Pangani, KM 50, China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara ya Tungumaa-Mkwaja-Mkange KM 95.4 na M/s Shandong Luqiao Group Ltd anayejenga daraja la Pangani mita 525 na barabara za maingilio takriban KM 25 mjini Pangani kufanya kazi kwa bidii na viwango vya juu ili kukidhi matarajio ya watanzania.
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua ushoroba wa mwambao wa bahari ya hindi na kukuza uchumi wa wakazi wa mikoa ya Tanga,Pwani na Dar es salaam.
Kwa upande wake Mbunge wa Pangani ambae pia ni Waziri wa maji Mhe. Jumaa Aweso ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa inaoufanya mkoani Tanga na kuwataka wananchi wa maeneo inapopita miradi ya ujenzi kuchangamkia fursa za ajira, ujuzi na biashara.
Naye meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Eng. Eliazary Rweikiza amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa wataalam wamejipanga vizuri kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora na kuleta tija kwa taifa.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku mbili mkoani Tanga kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja ikiwa ni mkakati wa kuwakumbusha wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wakati huu ili kuepuka visingizio vya kuchelewesha miradi pindi mvua za vuli zitakapoanza kunyesha baadae mwezi Oktoba.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI
EmoticonEmoticon