NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, SABASABA
WANACHAMA
wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) hususan Wastaafu
wameelezea kuridhishwa kwao na huduma wanazozipata hivi sasa kutoka kwenye
Mfuko huo ambao Agosti Mosi, 2023 utatimiza miaka Mitano tangu uanzishwe baada
ya Serikali kuunganisha Mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, PPF, LAPF NA
GEPF.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti walipofika kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya 47 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Julai 5, 2023 walisema kero zilizokuwepo
miaka michache iliyopita kwa sasa hawakumbani nazo.
“Wakati
nafuatilia Mafao yangu nilihudumiwa vizuri, ofisi hii imebadilika sana
nawaombea kwa Mungu muendelee hivyo hivyo, nawapa hongera nyingi, nasema haya
kutoka moyoni mwangu, nimefika hapa na kupata huduma kwa haraka.” Alisema
Mstaafu Bw. Abdallah Mandwanga.
Bw.
Amana Shomari, Mstaafu kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) miaka 10 iliyopita
alisema kwa upande wake huduma anazozipata kwa sasa kutoka PSSSF zimeboreka
sana na zimekuwa za kutia moyo.
“Nikiwa
kama Mstaafu, kilichonileta hapa sabasaba kwenye banda hili la PSSSF, ni
kuhakiki taarifa zangu, nimetumia si zaidi ya dakika 5 kupata huduma, hakika
nawapongeza sana, nitoe wito kwa wastaafu wenzangu zoezi la uhakiki ni muhimu
kwani linaondoa ucheleweshaji wa malipo ya mafao, mimi sina tatizo na malipo
yangu ya kila mwezi, napokea kwa wakati haivuki tarehe 25 pesa nakutana nayo
kwenye akaunti yangu.” Alisema.
Naye
Bw. Stanslaus Kagaruki ambaye naye alifika kwenye banda la PSSSF amewahamasisha
wastaafu wenzake kuona umuhimu wa kuhakiki taarifa zao kwani licha ya kwamba ni
takwa la kisheria lakini ni huduma inayotolewa kwa muda mfupi.
“Nimechukua
muda mfupi sikutarajia, nilidhani itanichukua muda mrefu, kumbe ni dole gumba,
sekunde tu nimekamilisha, hivyo nawasihi wenzangu wafike kuhakikiwa ili
waendelee kupokea Pensheni bila ya kikwazo.” Alisema Bw. Kagaruki.
Akizungumzia
hali ya Mfuko kwa sasa, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema
Mfuko umeendelea kutekeleza majukumu yake kama yalivyo ainishwa katika sheria
ya Mfuko kwa umahiri na umakini mkubwa ambapo aliyataja majukumu hayo kuwa ni Kuandikisha
Wanachama, Kukusanya Michango na Kuwekeza Michango hiyo na Kulipa Mafao.
“Hadi
sasa tuna wanachama 780,000 na tunakusanya Michango kwa mwaka shilingi trilioni
1.65, na tunalipa Mafao shilingi trilioni 1.6 kwa mwaka,” alifafanua CPA.
Kashimba.
Akifafanua
zaidi Mkurugenzi huyo Mkuu wa PSSSF alibainisha kuwa, kwa sasa kuna jumla ya wanufaika
wa Mafao ya kila mwezi (Monthly Pension) wanaofikia 160,000 ambao wanaolipwa Pensheni
ya jumla ya shilingi bilioni 65 kila mwezi.
“Hapa
utaona jinsi Mfuko unavyochachua uchumi wa nchi kwani wazee wetu hawa
wanapopokea Mafao haya wanakwenda kununua huduma na mahitaji yao mbalimbali na
hivyo fedha nyingi zinawafikia wananchin huko mtaani.” Alifafanua.
Aidha
Mkurugenzi huyo Mkuu wa PSSSF amedokeza kuwa, Mfuko uko mbioni kuzindua mfumo
mpya wa Kidijitali utakaowezesha kushughulikia masuala yote ya mafao kwa njia
ya mtandao.
“Hakutakuwa
na sababu ya mstaafu kuzunguka ofisini kufuatilia mafao, mstaafu mtarajiwa atajaza
maombi akiwa kwenye meza yake ofisini na taarifa atakuwa anazipata kwenye simu
yake ya mkononi.
“Hii
yote inafanyika katika kuhakikisha tunasogeza huduma karibu kwa wanachama wetu
na wastaafu kwa ujumla ili kuwaondolea adha ya kuzunguka huku na kule
kufuatilia mafao yao, tunaamini kupitia mfumo huu ndani ya muda mfupi baada ya
kujaza taarifa zao zitachakatwa na muhusika atakutana na fedha zake benki,”
amesema Kashimba.
CPA. Kashimba amesema kupitia mfumo huo mfanyakazi anayekaribia kustaafu ataweza kujaza taarifa zake akiwa ofisini na zikachakatwa kwenye mfumo kisha kukutana na fedha zake benki.
Alisema
mafanikio yanayoonekana hivi sasa kwa sehemu kubwa yamechangiwa na juhudi kubwa
zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye tangu
ameingia madarakani Serikali imeongeza ajira kwa kiwango cha juu.
Wanachama
wa PSSSF ni watumishi wote wa Umma, kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na
Mashirika ambayo Serikali inamiliki Hisa zaidi ya asilimia 30%, alifafanua.
“Kwa
kasi hii ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuongeza ajira nchini, Mfuko
unatarajia ongezeko la wanachama na kufikia elfu 40 kwa mwaka.” Alifafanua.
Mwanachama wa PSSSF (kulia) akihudumiwa
EmoticonEmoticon