Na Oscar Assenga,Kilindi
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga, imewafikisha katika mahakama ya Wilaya ya Kilindi watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi waliopewa kazi ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za POS.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni wakusanyaji mapato ambao hawakuweza kuwasilisha makusanyo ya mapato kwa Afisa Mapato Wilaya ya Kilindi kinyume na kanuni za fedha za serikali za mitaa za mwaka 2009.
Watuhumiwa hao wanesomewa mashitaka na Mwendesha mashitaka wa serikali CPL Frank Pastory Maugo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi Mh. Musa Ngalu.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka matatu; kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu wa mali ya umma kinyume na vifungu vya 28(1) vya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007 sura ya 329 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Kosa la pili ni wizi kwa mtumishi wa umma kinyume na kifungu cha 270 na 265 ya sheria ya makosa ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022 na kosa la tatu ni kuisababishia hasara Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kwa kutowasilisha makusanyo ya mapato kwa mhasibu wa halmashauri kinyume na aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) ya sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya 2022.
Mshitakiwa wa kwanza ni Joyce Ikungu, mtendaji wa kijiji cha Songe ambaye amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi EC. Na. 8/2023 kwa kuisababishia hasara ya kiasi cha Tsh. 3,590,000/= halmashauri ya Wilaya ya Kilindi wakati akitimiza jukumu la ukusanyaji mapato ya Halmashauri hiyo.
Mshitakiwa wa pili ni Calvin Ombeni Lema Mtendaji kata ya Kimbe ambaye amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi EC. Na. 6/2013 kwa kuisababishia hasara Halmashauri kiasi cha TZS 4,528,100, mshitakiwa wa tatu ni Athumani Mohamed Mhina Mtendaji wa kijiji cha Masagalu ambaye amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi EC.Na 7/2023 kwa kusababisha hasara ya TZS 1,415,200, kwa halmashauri ya Wilaya ya Kilindi wakati wa utekelezaji jukumu la ukusanyaji mapato.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mpaka kesi itakaposomwa tena Juni 27, 2023 katika Mahakama ya Wilaya ya Kilindi, washitakiwa wote wameachiwa huru kwa dhamana.
Mwisho
EmoticonEmoticon