Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Abdul Mkeyenge akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma kuhusu kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu kuufanya mkoa Kigoma kuwa Kitovu cha uchumi kwa mikoa ya magharibi nchi za ukanda wa maziwa makuuBoti za abiria na mizigo zinazofanya safari kutumia ziwa Tanganyika
Na Mwandishi Wetu ,Kigoma
SHIRIKA la uwakala wa meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa limejipanga kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuufanya mkoa Kigoma kuwa kitovu cha biashara kwa mikoa ya magharibi na nchi za maziwa makuu kwa kuhakikisha wanasimamia kwa tija kubwa vyombo vya usafirishaji majini kwenye ziwa Tanganyika.
Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Abdul Mkeyenge wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma ambapo alisema kuwa mkoa Kigoma unayo tija kubwa ya kufanya biashara na shughuli za kiuchumi na nchi za maziwa makuu ambapo ziwa Tanganyika kwa sasa ndiyo njia kuu inayohudumia usafirishaji wa bidhaa na abiria kutoka na kuingia kwenye nchi hizo.
Kutokana na hali hiyo alisema kuwa TASAC imejipanga kuongeza maradufu watendaji wake mkoani Kigoma kuhakikisha shughuli zinazohusiana na taasisi hiyo na wasafirishaji majini zinashughulikuwa kwa urahisi kwa kipindi kifupi ili kusiwe na mkwamo kwenye utekelezaji wa shughuli za biashara na uchumi.
Mkeyenge alisema kuwa wamejipanga pia kuhakikisha taratibu za kisheria za kimataifa na zile za Tanzania za usalama wa usafirishaji majini ziwa Tanganyika kwa vyombo vinavyokwenda nchi za Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia zinatekelezwa kikamilifu.
“Zipo changamoto za usimamizi wa taratibu na sheria kwa wenzenu wa nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika ikiwemo meli na boti za abiria kuchanganya bidhaa hizo wakati sheria za Tanzania zinakataza bidhaa hizo mbili kuchanganywa hivyo vipo vikao na majadilinao yanaendelea ili kuliweka jambo hilo sawa,”Alisema Mkeyenge.
Akizungumzia mpango wa serikali wa kuufanya mkoa Kigoma kuwa kitovu cha biashara Mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji wa maboti mkoa Kigoma, Ibrahim Sendwe alisema kuwa jambo hilo ni muhimu na litachochea biashara na uchumi wa mkoa Kigoma.
Sendwe alisema kuwa wao kama wasafirishaji wa mizigo na abiria wapo tayari kushiriki kwenye mipango hiyo lakini wanapaswa kupewa uelewa wa fursa ambazo kwao wanaweza kuzitumia kuleta tija kwenye mpango huo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanasimamia taratibu za usalama wa usafirishaji abiria ikiwemo taratibu na sheria za usafirishaji wa abiria na mizigo ili shughuli zao zisipingane na maelekezo ya serikali.
Kwa upande wake Mmiliki wa boti zinazofanya shughuli zake ziwa Tanganyika, Almas Juma amemshukuru Raisi Samia kwa maboresho makubwa yanayofanywa kwenye bandari ya Kibirizi na miradi mikubwa kwa mkoa Kigoma kwenye sekta ya biashara na uchumi kwani imechochea shughuli za biashara na uchumi mkoani humo.
Hata hivyo Juma ameomba serikali ya Rais Samia kuondoa tozo ya Viza inayotozwa kwa wasafiri wanaoingia mkoani Kigoma kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na ada ya dola 20 kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawana nyaraka za kufanya biashara.
EmoticonEmoticon