NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Wadau wa sekta ya mizani nchini wameiomba Serikali kuangalia upya gharama za uhakiki wa mizani pamoja na kuboresha mazingira ya biashara ili kuwawezesha wazalishaji wa ndani kushindana kwa usawa na bidhaa zinazoingia nchini kwa njia zisizo rasmi.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa wadau wa sekta ya mizani ambapo washiriki walieleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo gharama za uzalishaji, ada za uhakiki wa mizani na ushindani kutoka kwa bidhaa zinazouzwa bila kufuata taratibu za kisheria.
Akizungumza katika mkutano huo leo Juni 16, 2026 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ilala (WMA), Muhono Nashon, amesema bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya mizani iliyohakikiwa na kuidhinishwa na mamlaka husika.
Amesema kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya mizani na vipimo, baadhi ya watumiaji hukimbilia bidhaa za bei nafuu bila kuzingatia ubora, usalama na uhalali wake, hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa soko la bidhaa zisizokidhi matakwa ya sheria.
Kwa upande wake, mdau wa mizani Gilbert Mabati amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazowakwamisha wazalishaji wa ndani, akisisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala yanayohusu mazingira ya biashara ili kuongeza tija na ushindani katika sekta hiyo.
Naye muuzaji wa mizani ya kupimia mazao, Suleiman Baruti, amesema sheria zinamtaka kila mzalishaji au muuzaji kuhakikisha mizani imehakikiwa kabla ya kuuzwa kwa mteja ili kulinda maslahi ya watumiaji na kuhakikisha usahihi wa vipimo.
Amesema bado kuna baadhi ya mizani inayouzwa sokoni bila kufanyiwa uhakiki, hivyo kuwataka wazalishaji na waagizaji kuzingatia kikamilifu taratibu za uhakiki wa vifaa vya vipimo kabla ya kuviingiza katika soko.
Kwa upande wake, mdau mwingine wa sekta hiyo, William Mwalomba, amesema wazalishaji wa ndani wanabeba gharama kubwa za uzalishaji, upatikanaji wa vibali na uhakiki wa mizani, lakini bado hukabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia za magendo na kuuzwa kwa bei ya chini.
Amesema hali hiyo huwafanya baadhi ya wanunuzi kuvutiwa na bidhaa hizo kutokana na kukosa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kutumia mizani iliyohakikiwa na kuthibitishwa na mamlaka husika.
Kutokana na changamoto hizo, Mwalomba ameiomba Serikali kupunguza ada ya uhakiki wa mizani inayozalishwa nchini kutoka Shilingi 7,000 hadi Shilingi 4,000 kwa kila kifaa, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha viwanda vya ndani, kuongeza ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
EmoticonEmoticon