Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli
akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa
barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akikata
utepe ishara ya uzindua wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa
kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018.
Mbunge
wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto
Mashaka Biteko akimshuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt John Pombe Magufuli kwa fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya
ujenzi wa shule na vituo vya afya Wilayani bukombe wakati wa dhifa ya
uzinduzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018.
Mamia
ya wananchi Wilayani Bukombe Mkoa wa Geita wakimlaki Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli mara baada ya
kuzindua barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45, Leo Jumamosi 10 Machi 2018.
Na Mathias Canal, Ushirombo-Geita
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Leo
Jumamosi 10 Machi 2018 amezindua rasmi barabara ya Uyovu-Bwanga yenye
urefu wa kilomita 45 ambayo imekamilika kwa kujengwa kwa kiwango cha
lami.
Katika
dhifa hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Runzewe Kata ya Uyovu Wilaya
ya Bukombe Mkoani Geita, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ni nchi ya
tano kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika hivyo wananchi wanapaswa
kuwapuuza wanasiasa wanaohubiri kuporomoka kwa uchumi kwa matakwa ya
kujiimarisha kisiasa.
Alisema
katika kipindi cha miaka miwili serikali imefanya kazi kubwa ikiwa ni
pamoja na kuimarisha sekta mbalimbali kwa usimamizi nzuri katika
rasiliamali Madini, kuboresha sekta ya elimu ambapo wanafunzi wanasoma
bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.
Alisema
kuwa, bajeti ya mwaka 2015 katika sekta ya afya ilikuwa ni Bilioni 31
lakini serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha afya za watanzania
ambapo sasa bajeti imefikia shilingi Bilioni 239 na hayo ni matokeo ya
umoja na amani iliyopo nchini.
Rais
Magufuli amesema amani iliyopo nchini Tanzania imejengwa chini ya
uasisi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikasimamiwa vyema na
marais wastaafu Mhe Ally Hassan Mwinyi, Mhe Benjamin Mkapa pamoja na Mhe
Jakaya Mrisho Kikwete.
"Mambo
yanayofanywa na serikali hayawezi kuyafurahisha mataifa mengine hivyo
mataifa hayo yanawatumia watanzania wenyewe kutengeneza chuki dhidi ya
serikali yao" Alikaririwa Rais Magufuli
Aliongeza
kuwa kukamilika kwa barabara hiyo imekuwa sehemu ya Kuchochea shughuli
za maendeleo ya kijamii katika usafirishaji wa mazao, kurahisisha
usafirishaji wa watu na bidhaa, sambamba na kuongeza pato la Mkoa wa
Geita na Taifa kwa ujumla.
Katika
hatua nyingine Rais Magufulu amewasihi wananchi Kutovamia hifadhi za
Taifa badala yake kuwa wavumilivu na kuiacha serikali ifanye, kwani
watatumwa wataalamu wa Wizara ya ardhi na maliasili ili kuratibu na
kuona namna ya kuyagawa maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima.
Naye,
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe Elius John Kuandikwa na Mtendaji Mkuu wa
Tanroads nchini Mhandisi Patrick Mfugale walisema kuwa usanifu wa
barabara hiyo ulifanywa mwaka 2006 na kampuni mbili za kitanzania kwa
jumla ya Shilingi Milioni 207.6 ambapo barabara hiyo imesanifiwa kubeba
na kutumika kwa miaka 20 kwa upana wa mita 9.5
Walisema
Ujenzi wa barabara hiyo uliokamilika Octoba mwaka jana umegharimu jumla
ya shilingi Bilioni 45.454, ambapo msimamizi amelipwa shilingi Bilioni
2.3 huku akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi mwezi
Octoba mwaka huu.
Dhifa
ya uzinduzi wa barabara hiyo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mhandisi Robert Gabriel, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano, Mhe Elius John Kuandikwa, Mbunge
wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto
Mashaka Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Tanroads
Mhandisi Patrick Mfugale.