Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wananchi Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga wakati wa dhifa ya uzinduzi wa barabara ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita 132, Leo 10 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Sehemu ya mamia ya wananchi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa barabara ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita 132, Leo 10 Machi 2018.
Na Mathias Canal, Kahama-Geita
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Leo 10 Machi
2018 amezindua barabara ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita
132 iliyojengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami.
Katika
sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo katika Eneo la Nyasubi, Kahama Mjini Mhe
Rais Magufuli amesema kuwa Barabara hiyo ni chachu ya ukuaji wa uchumi na
kiungo cha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera pia ni sehemu ya kurahisisha
na kuimarisha mahusiano chanya ya kibiashara baina ya nchi za Uganda, Rwanda na
Burundi.
Rais
Magufuli amewataka wafanyabiashara nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya
dawa kwani serikali inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 269 kununua dawa nje ya
nchi hivyo endapo watajenga viwanda hivyo vya dawa serikali itawanufaisha
wafanyabiashara wa ndani ya nchi kwa kununua bidhaa hizo.
Kama
alivyojipambanua katika kuwatetea wanyonge Mhe Rais Magufuli ameagiza kutohamishwa
wananchi waliovamia eneo la ardhi ya Wizara ya Elimu, wilayani Kahama Mkoa wa
Shinyanga lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (MWAMVA), na kusema kuwa wananchi hao ndio waliompigia kura na hatimaye kuwa Rais wa nchi hivyo hawapaswi
kunyanyaswa.
Aidha,
aliwataka wananchi wengine kutoendelea na ujenzi wa nyumba za makazi katika Mtaa
wa Igomelo, Kata ya Malunga ili eneo lililosalia la hekari 40 ndilo litumike
kujenga chuo hicho.
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli amewashukuru wabunge wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana
na wabunge wengine wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha
sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 ambayo
inataka kuwa na uchumi fungamanishi kwa wananchi kupitia rasilimali zao.
Aidha,
serikali imekuwa ikikusanya mapato mengi kupitia sekta ya madini ambapo mwaka
2014/2015 ilikusanya jumla ya shilingi Bilioni 168.09, mwaka 2015/2016
ilikusanya zaidi ya Bilioni 205, mwaka 2016/2017 ikikusanya jumla ya Shilingi
Bilioni 213.365
Katika
hatua nyingine Diwani wa Kata ya Bugalama (CHADEMA), Katibu mwenezi Kanda ya
ziwa (CHADEMA) na wanachama wengine 50 wamejivua uanachama wa Chadema mbele
ya Rais Magufuli na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi huku wakisema kuwa
wameridhishwa na utendaji wake katika kuwatumikia watanzania.
Mradi
wa ukarabati wa barabara hiyo ya Isaka-Ushirombo yenye urefu wa Kilomita
132 iliyojengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami ni sehemu ya barabara
kutoka Isaka hadi Lusumo yenye kilomita 1334 iliyokuwa imejengwa mwaka 1980 na
mwanzoni mwaka 1990 hivyo imetumika kwa kipindi cha miaka 20 bila kufanyiwa marekebisho.
Dhifa
ya uzinduzi wa barabara hiyo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe
Zainab Telack, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano, Mhe Elius John Kuandikwa (Mb), Naibu waziri wa Madini
Mhe Doto Mashaka Biteko (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Tanroads
Mhandisi Patrick Mfugale, na Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga.