Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye mazungumzo
na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea
Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini
Seoul Korea Kusini wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu ya Waziri
Mahiga nchini humo.
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake
kwenye mazungumzo na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber
of Commerce and Industries (KCCI).
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye picha
ya pamoja na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of
Commerce and Industries (KCCI). Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania
nchini Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Matilda Masuka.
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye picha
ya pamoja na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of
Commerce and Industries (KCCI). Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania
nchini Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Matilda Masuka.
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake
kwenye mazungumzo na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber
of Commerce and Industries (KCCI)
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA NCHINI KOREA KUSINI, AAHIDI USHIRIKIANO WENYE TIJA KWA MAENDELEO YA WANANCHI WOTE
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameahidi kusimamia uimarishwaji wa uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ili wananchi wa pande zote mbili wapate manufaa.
Waziri Mahiga ameyasema hayo alipokuwa
anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu ambapo siku ya mwisho
aliitumia kikamilifu kukutana na taasisi za umma za biashara na viwanda,
Benki ya Exim ya Korea pamoja na makampuni binafsi yanayojipanga kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Amesema kuwa miaka 25 ya kwanza ya
uhusiano wetu na Jamhuri ya Korea ilijikita kwenye kuweka misingi imara
ya uhusiano wa kidiplomasia ambapo nchi zetu zilikuwa zinajiimarisha
kama mataifa huru. “Sasa ni wakati wa kushamiri kiuchumi tuone sekta binafsi zinavyoshiriki
katika kukuza uchumi, wananchi wa Tanzania waje kwa wingi nchini Korea
kujifunza masuala ya teknolojia, uhandisi na hata usanifu na ubunifu.
Huu ndio uhusiano wenye tija kwa mataifa yetu”. Mheshimiwa
Waziri alisema.
Akizungumza na Bw. Chang Yaong Hun,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea, Mheshimiwa Mahiga mbali
na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kutoa mikopo na misaada nchini
Tanzania, Waziri Mahiga alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa
John Pombe Magufuli sasa imejikita kwenye mapambano dhidi ya rushwa
na ujenzi wa viwanda ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu.
Kwasasa Benki hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme
na maji mikoa mbalimbali ya Tanzania ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mahiga alifafanua kuwa
ajenda ya Mheshimiwa Magufuli ya viwanda, haiwezi kukamilika bila kuwa
na miundombinu ya msingi kama vile uzalishaji wa umeme wa kutosha na
ukuaji wa sekta ya uchukuzi na mawasiliano ambapo Korea Kusini ni wabobezi
kwenye masuala hayo.
Alitumia fursa hiyo kumkaribisha
Bw. Chang na timu yake kwenda Tanzania kufanya tathmini ya miradi tunayoshirikiana
nao, lakini pia miradi mipya kwenye sekta ya uchukuzi kama ujenzi wa
Standard Railway Gauge “SRG” kutoka Isaka hadi Kigali, n.k. ambayo
ni miradi ya kipaumbele kwa sasa kwa taifa letu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Chang
alisifu utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli, na Serikali ya awamu
ya tano ya Tanzania na kusema kuwa utendaji kazi wa aina hii ni wa kupigiwa
mfano barani Afrika, na umekuja wakati muafaka tunapoingia kwenye hatua
nyingine ya uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi zetu mbili. Aidha aliongeza
kuwa, wakati umefika sasa wa kufanya kazi, nay eye yuko tayari kufanya
kazi na Tanzania kwani Serikali yake, imetoa kipaumbele kwa nchi hii.
Korea Exim Bank ni taasisi ya Serikali
inayosimamia mikopo na misaada ya Jamhuri ya Korea inayotoa kwa nchi
nyingine. Katika kipindi cha miaka minne (tangu 2016 hadi 2020), Korea
Kusini kupitia taasisi hiyo, imeongeza mikopo ya maendeleo kwa bara
la Afrika kwa asilimia 20. Uamuzi wa Serikali iliyokuwa madarakani mwaka
2016 wa kuichagua Tanzania kupokea kiasi kikubwa cha msaada huo kuliko
nchi nyingine ya Afrika, umeendelezwa na Serikali iliyopo sasa madarakani
ya Mheshimiwa Moon Jae-in, Rais wa Jamhuri ya Korea.
Ujumbe wa Mheshimiwa Augustine Mahiga
pia ulikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Judong Kim, Makamu Mwenyekiti
wa Chemba ya Biashara na Viwanda ya Korea (Korea Chamber of Commerce
and Industries KCCI), ambapo Waziri Mahiga aliwasisitiza kuja Dar es
salaam kuangalia fursa zilizopo ili kuwashawishi wanachama wao kutafuta
bidhaa na masoko nchini Tanzania.
Akielezea umuhimu wa KCCI kuzuru
Tanzania na kujifunza soko la biashara, Bw. Edwin Rutageruka Mkurugenzi
Mkuu wa TANTRADE aliyeongozana na ujumbe wa Mheshimiwa Waziri Mahiga,
alisema njia nzuri ya kupata picha halisi ni kupitia Maonesho ya Biashara
ya Saba Saba. Hivyo alitumia fursa hiyo kualika ujumbe wa KCCI kushiriki
kwenye maonesho ya 42 yanayotarajiwa kuanza tarehe 28 Juni – 10 Julai,
2018.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake,
Mheshimiwa Mahiga pia alikutana na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu
wa makampuni ya DOHWA, ambao wamejikita kwenye ujenzi na ukarabati wa
miundombinu ya reli n.k. Makampuni mengine ni KORAIL, STX Engine, KTMI
& STX Offshore pamoja na GS E&C, ambao wote wameonesha nia ya
kuwekeza au kufanya biashara nchini Tanzania. Ujumbe mkuu kwa taasisi
na makampuni hayo ulikua ni kupanua fursa za ushirikiano wa biaashara
na uwekezaji, ubadilishanaji wa ujuzi na ujengaji uwezo wa wafanyakazi
ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu.
Pamoja na kuzungumza na makampuni
ya umma na sekta binafsi yaliyoorodheshwa hapo juu, ziara ya Mheshimiwa
Augustine Mahiga, ilimuwezesha kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la
Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ambapo alihutubia
mamia ya wafanyabiashara wa Korea kuhusu utayari wa Tanzania kushirikiana
na nchi hiyo kibiashara.
Mkutano huo uliopewa kauli mbiu ya
“Eplore Tanzania” ulifuatiwa na mikutano midogo midogo iliyowakutanisha
baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Korea Kusini ili kuangalia
kwa ukaribu maeneo ya ushirikiano. Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini
na mwenzake wa Korea Kusini nchini Tanzania wameazimia kuendeleza makongamano
hayo ya kila mwaka ili kuwa na ushirikiano wa karikiano wa karibu wa
kibiashara kwa mataifa hayo mawili kwa maendeleo ya wananchi wote.
Wajumbe wengine walioongozana na
Mheshimiwa Waziri Mahiga nao walipata fursa ya kuhutubia hadhara hiyo
kuhusu Tanzania ambapo Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania
Investment Centre alitoa utangulizi kuhusu uwekezaji Tanzania; Kanali
(mstaafu) Joseph Simbakalia, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA alizungumzia maeneo
ya kipaumbele kwenye maeneo maalum ya uwekezaji nchini Tanzania. Naye
Bi. Nasriya Nassor, Mkurugenzi wa Biashara wa Taasisi ya Uwekezaji Zanzibar
alitoa taarifa fupi kuhusu Zanzibar kama kivutio cha utalii ndani ya
Tanzania na eneo linalopendelewa na watalii wengi duniani.
Jamhuri ya Korea, kama inavyojulikana
rasmi na Umoja wa Mataifa, ni mojawapo ya nchi zinazofanya vizuri zaidi
duniani kiuchumi kwa sasa. Viashiria vya uchumi vinaonyesha uchumi wa
nchi hiyo utaendelea kukua kwa viwango kutokana na jitihada za dhati
za viongozi wa nchi hiyo za kufuta kabisa umaskini kwa wananchi wao.
Kwa sasa wastani wa pato kwa mtu “per capital income” inakadiriwa
kuwa zaidi ya US$ 34,000, ukilinganisha na US$ 22,670 mwaka 2012. Baada
ya vita ya Korea kwenye miaka ya mwanzo ya 1950, nchi ya Korea Kusini
ilikua maskini kuliko nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Tanzania ambapo
wastani wa pato kwa mtu ilikua na US$67.
Mheshimiwa Mahiga anatarajiwa kurejea
nyumbani baada yakuhitimisha ziara hiyo aliyosema italeta faida sio
tu kwa wafanyabiashara, ila kwa jamii kwa ujumla. “Nchi hii ni tajiri
sana kiuchumi; lakini utajiri wake mkubwa pia uko kwenye taaluma ya
rasilimali watu, hivyo kwa Tanzania kufanikiwa kufungua ubalozi hapa,
sasa tumefungua milango ya ushirikiano wa karibu, kuliko ilivyokuwa
mwanzo. Tuchangamke tuige mfano wa uchapa kazi wao, na sisi tutaondoka
kwenye umasikini” Waziri Mahiga alisema kwa umaliza,
kabla ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon, uliopo mjini
Seoul, Jamhuri ya Korea.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul, Korea Kusini,