Na: Veronica Kazimoto,
Dar es Salaam,
Wito
umetolewa kwa wananchi wote kuanza kulipa Kodi ya Majengo ya mwaka
2017/18 mapema kwa kuwa ulipaji wa kodi hiyo umerahisishwa ambapo
wanaweza kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Charles Kichere alisema hakuna muda utakao ongezwa
ifikapo Juni 30, mwaka huu na badala yake faini itatozwa kwa kila
mmiliki wa jengo atakayechelewa kulipa kodi hiyo.
“Kama
mamlaka hatuoni sababu ya kuongeza muda wa kulipa Kodi ya Majengo
ifikapo tarehe 30 Juni 2018 kwasababu tumewarahisishia wananchi ulipaji
wa Kodi hii ambapo wanaweza kupata ankara ya malipo kwa majengo
yaliyosajiliwa kwenye tovuti ya TRA au simu ya mkononi na kufanya malipo
katika tawi lolote la Benki ya NMB au CRDB popote nchini au kwa njia ya
mitandao ya simu ya Mpesa, Tigopesa au Halopesa”, alisema Kichere.
Kamishna
Mkuu Kichere alisema kuwa, wananchi wafuatilie matangazo ya namna ya
kulipa Kodi ya Majengo kwa njia ya kielektroniki katika mitandao ya
kijamii na kwenye vyombo mbalimbali vya habari au wafike katika ofisi za
TRA zilizo karibu na maeneo yao nchi nzima wapate utaratibu wa kulipa
kodi hiyo kielektroniki.
Kichere
aliongeza kuwa Kodi ya Majengo inalipwa kwa mujibu wa Sheria hivyo, ni
muhimu wananchi walipe mapema kodi hiyo ili kuepuka usumbufu unaoweza
kujitokeza mwishoni ikiwa ni pamoja na msongamano wa watu.
“Natoa
wito kwa wananchi kwamba, wasisubiri mpaka mwisho ndio waanze kupanga
foleni kwenye ofisi za TRA, wanatakiwa kulipa kuanzia sasa hivi katika
ofisi zetu na wanaweza kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki kama
nilivyoeleza hapo awali, kinyume na hapo itatubidi tutoze faini kwa
atakayechelewa kulipa kodi hii ya majengo,” alisisitiza Kichere.
Kodi
ya Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai mosi ya mwaka wa fedha husika
hadi Juni 30 ya mwaka unaofuatia kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu,
hivyo, muda huu ni muafaka kwa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo
mpaka ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.