CHATANDA AWAWASHIA 'MOTO' WAHANDISI WA MAJI HALMASHAURI YA MJI KOROGWE

February 28, 2018

PICHANI: Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga (CCM) Mary Chatanda (kushoto) leo Februari 28, 2018 amefika Mtaa wa Kwanduli, Kata ya Bagamoyo katika Halmashauri ya Mji Korogwe kuangalia miradi mbalimbali ikiwemo ule wa umeme kwenye vitongoji sita vya Mtaa wa Kwanduli unaotekelezwa kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Pichani anaangalia nguzo ambapo wakati wowote zitasimikwa. (Picha na Yusuph Mussa).

Na Yusuph Mussa, Korogwe
IMMAMATUKIO

MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda amesema kitendo cha wananchi wa Kitongoji cha Kwatomokwe, Mtaa wa Kwanduli, Kata ya Bagamoyo katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga kuwekewa vilula vya kuchotea maji, wakati maji hayo hayatoki, huo ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Alisema chanzo cha kukosekana maji hayo ni kutega mabomba kwenye vyanzo vya maji ambavyo havina uhakika, ndiyo maana mradi huo uliokamilika katikati ya Januari, mwaka huu, ulitoa maji siku ya ufunguzi, lakini baada ya hapo, maji hayajatoka tena.

Chatanda aliyasema hayo leo Februari 28, 2018 kwenye siku yake ya kwanza ya ziara ya siku 14 kwenye jimbo lake, ambapo leo alianza kwa kutembelea kata ya Bagamoyo kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.

"Hatuwezi kuwawekea wananchi mabomba ya maji pamoja na vizimba (vilula) vya maji, halafu maji hayo yasitoke, huko ni kuwadanganya wananchi, lakini sijajua utaalamu wa wataalamu wetu, hata ningekuwa mimi, nisingeweka mtandao wa mabomba ya maji kutokea Mto Mbeza, ule sio mto wa kutumainiwa, kwani maji yake yanakuwepo wakati wa masika tu.

"Nawaagiza wataalamu, tafuteni njia zozote hata kama ni za mgawo, wananchi wa Kitongoji cha Kwatomokwe nao wapate maji. Lakini pia kuna miradi miwili ya maji kutoka Mto Pangani, basi mjiandae kuwaunganishia maji wananchi pindi mradi huo utakapokamilika" alisema Chatanda.

Chatanda anewatoa wasiwasi wananchi wa Mji wa Korogwe na viunga vyake, kuwa wapo imara kuona miradi mikubwa miwili ya sh. milioni 500 kila mmoja, kuanzia ule wa Mtonga na Old Korogwe inakamilika mwaka huu na kuondoa kabisa tatizo la maji kwenye mji huo. Lakini pia Serikali imewapa sh. bilioni 2.5 za maji.

"Tatizo la maji katika Mji wa Korogwe tunaanza kulipatia ufumbuzi, ambapo Mradi wa Maji Mtonga unaojengwa kwa sh. milioni 500 utakapokamilika mwaka huu, utaweza kuhudumia wananchi wa Mtaa wa Mtonga na Msambiazi katika Kata ya Mtonga, lakini maji hayo pia yatafika katikati ya mji kwa kujenga tenki Mtaa wa Mlimafundi.

"Lakini kwa Mradi wa Maji Old Korogwe ambao nao utajengwa kwa sh. milioni 500, utaweza kupeleka maji kwenye mitaa ya Lwengera-Darajani na Lwengera-Relini. Pia mradi huo utaweza kufikisha maji Kata za Kilole na Bagamoyo, na hata maji hayo kuwafikia wananchi wa Kitongoji cha Kwatomokwe" alisema Chatanda.

Akizungumzia changamoto kwenye Kata ya Bagamoyo, Chatanda alisema tayari Serikali imeanza kupeleka nguzo kuona vitongoji vyote sita vya Mtaa wa Kwanduli vinapata umeme, tofauti na awali, ambapo ni vitongoji vichache ndiyo vilikuwa vipate umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

"Wananchi, nadhani wote mnakumbuka. Nilipokuja na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, nilizuia umeme usiwashwe mpaka vitongoji vyote sita vipate umeme, leo hii tayari nguzo zinasambazwa kwa ajili ya kuwekewa umeme, ambapo awali REA walileta nguzo 160 na sasa wameleta nguzo 216.

Kaimu Mhandisi wa Maji Halmashauri ya Mji Korogwe Raphael Mmasa alikiri maji hayo hayatoki kwenye vilula viwili kati ya vitatu kwenye kitongoji hicho, lakini tatizo ni ukame na kukauka Mto Mbeza.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Dkt. Elizabeth Nyemi alikiri upungufu wa maji kwenye Kitongoji cha Kwatomokwe na ameahidi kushughulikia changamoto hiyo.

Miradi mingine ambayo Chatanda ametembelea ni ujenzi wa Soko la Kimataifa linalojengwa pembeni ya Stendi Kuu ya Mabasi Kata ya Bagamoyo, Kituo cha Afya Bagamoyo, madarasa mapya matano na ofisi ya walimu kwenye Shule mpya ya Msingi Kilole na Shule ya Msingi Bagamoyo kuangalia ujenzi wa madarasa mawili.


Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga (CCM) Mary Chatanda akiwa amekata tamaa baada ya leo Februari 28, 2018 kupelekwa kuangalia mradi wa maji ya bomba ambao hautoi maji kwenye Kitongoji cha Kwatomokwe, Mtaa wa Kwanduli, Kata ya Bagamoyo katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Pamoja na kujigeuza Tomaso wa kwenye Biblia kwa kujaribu kufungua, pia bado maji hayo hayakutoka. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga (CCM) Mary Chatanda (kushoto) akiwa amekata tamaa baada ya leo Februari 28, 2018 kupelekwa kuangalia mradi wa maji ya bomba ambao hautoi maji kwenye Kitongoji cha Kwatomokwe, Mtaa wa Kwanduli, Kata ya Bagamoyo katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Korogwe Dkt. Elizabeth Nyema. (Picha na Yusuph Mussa).
<!--[if gte mso 9]> ...

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »