Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiahirisha
Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar katika Majengo
ya Baraza hilo yaliopo Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi
ya Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia
Hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipotoa Hoja
ya Kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar .
Baadhi
ya Manaibu Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wakimsikiliza Balozi Seif alipokuwa akisoma Hotuba ya Kuahirisha
Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar M,h. Zubeir Ali Maulid
akiongozwa na Askari wa Baraza hilo wakitoa nje ya Ukumbi baada
kufungwa kwa Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko
Chukwani.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo
na Mwakilishi wa Jimbo la Dimani Dr. Mwinyihaji Makame Mwadini baada ya
kufungwa kwa Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika mapambano yake dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia
vilivyokithiri katika maeneo mbali mbali Nchini, kamwe haitamvumilia,
kumuonea aibu, wala muhali Mtu yeyote wa cheo chochote na ngazi yeyote
pindi atakapobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Tisa la
Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika Majengo ya Baraza hilo
Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya na kutahadharisha wazi kwamba
Viongozi na Wananchi wanapaswa kutambua kuwa Sheria ni Msumeno.
Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kuchukuwa hatua kali za
kisheria dhidi ya wote watakaobainika kushiriki katika kadhia hiyo
ikiwemo wafanyaji na wale wote wanaoshiriki katika kuwalinda na
kuwakingia kifua wahalifu wote wa masuala ya udhalilishaji wa kijinsia.
Alivinasihi vyombo vya ulinzi na usalama kupambana zaidi dhidi ya
vitendo hivyo vinavyolitia aibu Taifa sambamba na kuharibu maisha ya
Wananchi, huku Jamii ikipaswa kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo
hivyo katika Mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo baya Kijamii na hata
Kidini.
Balozi Seif alisema tabia ya baadhi ya Watu hasa Familia kuzimaliza
kesi za Udhalilishaji Majumbani itakupunguza kasi ya Serikali
kuwashughulikia wahalifu hao na kuwanasihi Wananchi wahusika kufika
Mahakamani kwa kutoa ushahidi utakaotoa nguvu ya sheria kuchukuwa mkondo
wake na haki kupatikana ili hatimae kuvimaliza vitendo hivyo katika
Taifa hili.
Alieleza kwamba Baraza la Wawakilishi tayari limeshapitisha Sheria ya
adhabu kwa wahusika wa vitendo vya udhalilishaji, ambapo imeweka bayana
kuwa Mtuhumiwa ye yote wa kosa la udhalilishaji hatopaswa kupewa
dhamana.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Sheria hiyo sasa inangojea kuwekwa saini
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili iwe Sheria
ambapo Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuifanya kazi hiyo muda sio mrefu
kuanzia hivi sasa.
Akizungumzia suala la ulipaji umeme kwa Deni ya Shirika la Umeme
Tanzania {TANESCO} kwa upande wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alisema Serikali ililiamuru Shirika la Umeme Zanzibar
{ZECO}kulilipa deni hilo kwa Tanesco kwa kiwango cha Shilingi Bilioni
Mbili kwa Mwezi.
Alisema malipo hayo yamepangwa kwenda sambamba na Wizara ya Fedha na
Mipango Zanzibar pia kuagizwa kupunguza Deni hilo kwa kiwango cha
Shilingi Bilioni Moja kwa Mwezi malipo ambayo yalianza utekelezaji wake.
Hata hivyo Balozi Seif alieleza kwamba utekelezaji huo ulikumbwa na
changamoto zilizojitokeza kwa upande wa Shirika la Umeme Zanzibar
{ZECO} kwa kutoendelea kulipa kwa ukamilifu kiwango kilichowekwa na
Serikali na badala yake Shirika lililipa kwa Miezi Minne tu kuanzia
Mwezi Juni, 2017 hadi Oktoba, 2017.
Alisema Miezi iliyofuata ZECO ililipa Deni hilo chini ya kiwango
kilichoagizwa kutokana na ukusanyaji mdogo wa mapato yanayotokana na
ankara za matumizi ya umeme kutoka kwa baadhi ya Taasisi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na zile za Muungano wa Tanzania zilizopo Zanzibar.
Balozi Seif alisema hali hiyo imepelekea Shirika la Umeme Zanzibar
kutokuwa na mapato ya kutosha kulipa deni hilo kila Mwezi badala ya
kukidhi mahitaji mengine ya msingi na ya lazima ya kuliendesha Shirika
hilo.
Kuhusu suala la upatikanaji wa huduma za Maji safi ya salama Mjini na
Vijijini, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema
Serikali Kuu kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imejipanga
kutekeleza miradi Minne mikubwa ya huduma hiyo Nchini.
Aliutaja ule Mradi wa Uimarishaji wa Miundombinu katika kubadilisha
Mabomba yaliyochakaa wenye urefu wa Kilomita 68 katika Maeneo ya
Bumbwisudi, Kinumoshi, Kianga, Welezo, Muembe Mchomeke, Amani pamoja na
Kiponda Mji Mkongwe.
Alisema utekelezaji wa Mradi huu unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya
Afrika wa Awamu ya 12 {ADF 12} unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi
za Kitanzania Bilioni 48 hadi kukamilika kwake.
Balozi Seif aliutaja mradi mwengine wa Uimarishaji wa miundombinu ya
Maji Mjini unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 225 za Kitanzania utahusisha ujenzi wa
Matangi ya kuhifadhia Maji katika maeneo ya Welezo juu pamoja na Welezo
Magharibi.
Alieleza Mradi huo utakwenda sambamba na ulazaji wa Mabomba yenye urefu
wa Kilomita 120 katika Zoni ya Migombani pamoja na uwekaji wa huduma za
Umeme katika maeneo husika.
Balozi Seif alisema upo mradi mpya wa uimarishaji miundombinu ya Maji
Mjini utakaofadhiliwa na Serikali ya India kwa kwa gharama ya Shilingi
Bilioni Mia 207 utakaohusisha ulazaji wa Mabomba katika maeneo ya Zoni
ya Mfenesini, Kizimbani, Tunguu na Fumba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China imekubali kufadhili mradi wa uchimbaji Visima
11 pamoja na ulazaji wa Mabomba ndani ya Mkoa Kaskazini Unguja na
baadhi ya Wilaya ya Kati na Magharibi “A” unaotarajiwa kugharimu
shilingi Bilioni 12 za Kitanzania.
Alisema ili miradi yote iendelee kudumu kwa kipindi kirefu katika utoaji
wa huduma zake Wananchi watawajibika kuchangia gharama za uendeshaji wa
huduma hiyo kwa wale watakaopata badala ya kubakia na dhana ya
uchangiaji wa huduma ya Maji safi ni jukumu la Serikali pekee.
Mkutano wa Baraza la Wawakilishi ulipokea na kujadili Ripoti za Kamati
za kudumu Saba za Baraza hilo ambapo pia Wajumbe wa Baraza hilo
walijadili na kuipitisha Miswada Mitatu ya Sheria.
Miswada hiyo ni ule wa kufuta Sheria ya kusimamia mwenendo wa Biashara
na kumlinda mtumiaji ya Zanzibar Nambari 2 ya Mwaka 1995 na kutunga
Sheria Mpya ya Ushindani Halali wa Biashara na Kumlinda Mtumiaji, Kuweka
Masharti Bora zaidi pamoja na Mambo Mengine yanayohusiana na hayo.
Mwengine ni Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Adhabu na kutunga
Sheria Mpya ya Adhabu, Kuweka Masharti Bora zaidi pamoja na Mambo
Mengine yanayohusiana na hayo.
Mswada wa Tatu ni ule wa Sheria ya kufuta Sgeria ya Mwenendo wa Jinai
Nambari 7 ya Mwaka 2004 na kutunga Sheria Mpya ya Mwenendo wa Jinai na
kujweka utaratibu Bora wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Usikilizaji wa
Kesi za Jinai na Mambo Mengione yanayohusiana na hayo.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 9 Mwezi Mei Mwaka 2018.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/2/2018.