WAZIRI MKUU MAJALIWA AHIMIZA MFUMO WA ELIMU YA JUU UANDAE RASILIMALI WATU ILI KUFIKIA TAIFA LA UCHUMI WA KATI

December 03, 2017

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akimpongeza Balozi Nicolous Kuhanga mara baada ya kutunukiwa na Mhe Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, shahada ya heshima ya uzamivu kutokana na mchango wake mkubwa hasa wakati wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu Huria Tanzania.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim akimpongeza Mke wake Mama Mary Majaliwa mara baada ya kutunukiwa shahada ya uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera kutokana katika Chuo Kikuu Huria Tanzania mapema jana Mjini Singida.




                    Picha/habari na Nathanieli Limu-Singida

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa Kassim amesema kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa elimu ya juu nchini ili kuuboresha uweze kusaidia kutayarisha haraka rasilimali watu walioelimika  zaidi, watakaoliwezesha  taifa kuwa na maendeleo na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.


Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema huyo  wakati akizungumza kwenye kilele cha mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida. 
“Kwa kuzingatia malengo ya dira ya taifa ya maendeleo na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano, napenda nisisitize kuwa dira ya utendaji wenu ijikite katika maeneo yaliyoainishwa chini ya mwamvuli wa kauli mbiu ya chuo-elimu bora na nafuu kwa wote”, amesema. 
Amesisitiza kwa kusema kwa uchumi wa kati na wa viwanda, hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23. 



“Hivi sasa kiwango cha Tanzania cha udahili katika elimu ya juu ni aslimia nne (4). Kiwango hiki ni kidogo hata kuliko nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao licha ya hali ya vita nchini mwao kwa muda mrefu,wamefikia asilimia saba (7)”,amefafanua.
Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua zaidi kwa kusema kuwa takwimu zinaonyesha kwamba karibu nchi zote washiriki katika jumuiya ya Afrika mashariki, ukiacha Burundi, zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya juu ikilinganishwa na kiwango cha Tanzania. 
Amesema kwa mujibu wa sera ya elimu ya mwaka 2014 mfumo wa elimu na mafunzo umetawaliwa na muundo wa kitaaluma wenye dhana ya kuchuja wahitimu kwa kila ngazi ili kupata wachache wenye uwezo mkubwa katika taaluma.
“Hali hii inatokana na nafasi za elimu na mafunzo ngazi za juu kuwa chache kadri wanafunzi wanavyohitimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na kuendelea. Kwa uhaba wa nafasi za elimu ya juu na ufinyu wa bajeti ndio unaosababisha kutumia muundo wa kuchuja badala ule wa kutoa fursa kulingana na uwezo, vipaji na vipawa”, amesema na kuongeza;
“Huu ndio mfumo ambao unahitaji kuhuishwa na mfumo wa elimu huria na masafa kama alivyoeleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Profesa Joyce Ndalichako kwamba mazingira, vigezo na masharti ya mchakato huu vimeainishwa katika sera ya elimu na mafunzo 2014’. 
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inaunga mkono azma ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuanzisha dawati maalum kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa elimu huria na masafa.
“Kupitia hafla hii, ninaagiza dawati kama hili lianzishwe pia katika Tume ya vyuo vikuu (TCU) na Baraza la elimu ya ufundi (NACTE), kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zao za ithibati zinazingatia na kukidhi matakwa ya viwango vya mfumo wa elimu huria na masafa”, amesema.
Katika Mahafali hayo Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda amemtunuku shahada ya heshima ya uzamivu Balozi Nicolous Kuhanga ambaye mchango wake umetajwa kuwa mkubwa hasa wakati wa kuanzishwa kwa chuo hicho.
Zaidi ya wahitimu 2200 wamehitimu katika Chuo Kikuu hicho na kutunikiwa shahada mbalimbali ambapo mke wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Mama Mary Majaliwa, amekuwa miongoni mwa wahitimu akitunukiwa shahada ya uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »