WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa Onyo kwa watumishi wa umma na Madiwani wa
Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na akawataka
wajirekebishe mara moja.Ametoa onyo hilo jana (Jumamosi, Desemba
23, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa manispaa na madiwani kwenye
kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana
ya Songea, mjini Songea Mkoani Ruvuma
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
………………
*Aaagiza wahusika wachunguzwe
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la
Pamba (CDTF) na amegiza wahusika wote wachunguzwe ili kubaini fedha
walizokusanya zimetumikaje.
Alitoa
agizo hilo mwishoni mwa wiki (Ijumaa, Desemba 22, 2017) wakati
akizungumza na wadau wa zao hilo kwenye kikao alichokiitisha mkoani
Shinyanga kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo alikwishakuyatoa. Waziri
Mkuu alishafanya vikao vitatu na wadau mbalimbali wa zao hilo.
Alichukua
uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watendaji wa mfuko huo hawajatekeleza
majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo lakini pia majukumu yao yanaingiliana
na yale ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).
“Kuna
CDTF katika zao la pamba lakini hakuna inachofanya ambacho kinawalenga
wakulima moja kwa moja. Tunaiondoa CDTF na kazi zake kuanzia sasa
zifanywe na Bodi,” alisema.
“Waziri
wa Kilimo peleka timu ya ukaguzi kuona wamefanya nini hadi sasa.
Tunataka Bodi ifanye kazi na iulizwe maswali kuhusu zao hili. Endapo
kuna jambo halijafanyika, Bodi iwe na uwezo wa kutoa majibu si kusubiri
tena mtu wa chombo kingine aje kutoa majibu,” alisema Waziri Mkuu.
“Kwa muundo huu, Mkurugenzi wa Bodi anakaa tu, wakati akisubiri kazi yake ifanywe na CDTF,” aliongeza.
Mfuko
wa CDTF unaundwa na wajumbe sita ambao ni wawakilishi wa wakulima
wawili, wawakilishi wa wenye viwanda vya kuchambua pamba wawili,
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya
Kilimo.
Mfuko
huu uliundwa mwaka 1999 na Bodi ya Pamba (TCB) ili uwashirikishe wadau
wa zao hilo kuondoa matatizo yaliyojitokeza kwenye sekta hiyo baada ya
Serikali kujitoa kwenye uendeshaji wa moja kwa moja wa mazao nchini
ikiwemo uzalishaji na biashara kutokana na mfumo wa soko huria.
Desemba mwaka jana, Waziri
wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alifikia uamuzi kama huo na kuamua
kusimamisha shughuli zilizokuwa zinafanywa na Mfuko wa Kuendesha Zao la
Korosho Nchini (CIDTF) ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko huo.
Akitangaza
uamuzi huo jijini Dar es Salaam, Waziri Tizeba alisema hatua hiyo
ilichukuliwa baada ya mfuko huo kushindwa kutekeleza majukumu yake
kikamilifu pamoja na kuwapo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu utendaji
wa mfuko huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 24, 2017