WATAKAOKUTWA NA BIDHAA ZA MAGENDO MUHEZA KUSHTAKIWA KWA UHUJUMU UCHUMI

December 08, 2017

MKUU wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Mhandisi Mwanasha Tumbo amesema wananchi watakaokutwa na bidhaa za magendo kwenye nyumba zao watakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria wakishtakiwa kwa kosa la kuhujumu uchumi wa nchi.

Hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha biashara za magendo ambazo zimekuwa zikiingizwa wilayani humo kupitia bandari bubu ya Kigombe zinakoma ikiwa ni mkakati wa kukabiliana kwa vitendo ili kukomesha shughuli hizo ambazo zinaisababishia serikali kukosa mapato.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kigombe kata ya Kigombe wilayanu humo katika mkutano wa hadhara uliofanyika  kuhusiana na operesheni zinazoendesha na Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga kudhibiti biashara hizo ambazo zimekuwa kikwazo cha kukusanya mapato.

Alisema biashara za magendo vimekuwa na athari kubwa kwa ukuaji wa uchumi wanchi kutokana na kukosa mapato ambayo yangeweza kuwasaidia katika harakati mbalimbali za kimaendeleo kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Niwaambie tu tukija nyumbani kwako tukikuta dawa za kuleva na bidhaa za magendo tutawachukua watu wote watakaokutwa na kuwashtaki kwa kosa la uhujumu uchumi lakini hata wale watakaokuwa na dawa za kulevya watakamatwa “Alisema.

“Lakini pia niwatake wananchi mtoa ushirikiano kwa operesheni
inayoendelea kwenye eneo hili kwa kutoa taarifa ambazo zinaweza kusaidia kufanikisha suala la biashara za magendo na dawa za kulevya linatoweka kwenye maeneo yenu “Alisema.

Akizungumza katika mkutano huo mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Mohamed Khatibu alilalamikia kitendo cha askari kupekua nyumba zao kwa madai ya kusaka bidhaa za magendo kitendo ambacho sio kizuri.

“Kwa kweli kitendo cha askari kuja nyumbani kwetu na kuanza kutupekua tena bila kibali sio cha kiungwana hivyo tunaomba suala hilo lifanyiwe kazi na mamlaka zinazohusika “Alisema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »