Hussein Makame-NEC
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mdogo katika
majimbo ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini na kata sita za
Tanzania Bara ambao utafanyika tarehe 13 Januari mwaka 2018.
Akitoa
taarifa kwa umma jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Mhe.
Jaji Mkuu (Mst. Zanzibar) Hamid Mahmoud Hamid, alisema Tume imetangaza
uchaguzi huo kufuatia kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuwepo nafasi wazi ya jimbo la Singida
Kaskazini kufuatia kuvuliwa uanachama wa CCM mbunge wa jimbo hilo Lazaro
Nyalandu na hivyo kupoteza sifa ya kuwa mbunge.
Kwa
upande wa Jimbo la Songea Mjini, Jaji Mst. Hamid alisema kuwa Spika
aliitaarifu Tume kuwepo nafasi wazi ya jimbo hilo kufuatia kifo cha
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Leonidas Gama huku Tume ikipokea Hati ya
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ikithibitisha kuwa Jimbo la Longido kuwa
wazi baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo.
Aliongeza
kuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa kuzingatia masharti
ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura
ya 292, aliitaarifu Tume kuwepo nafasi wazi za madiwani katika kata sita
Tanzania Bara.
Mhe.
Jaji Mst. Hamid alizitaja kata zinazohusika katika uchaguzi huo kuwa ni
Kimandolu (Halmashauri ya Jiji la Arusha), Kihesa (Halmashauri ya
Manispaa ya Iringa), Bukumbi (Halmashauri ya Wilaya ya Uyui), Kurui
(Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe), Keza (Halmashauri ya Wilaya ya
Ngara) na Kwagunda (Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe).
Alisema
utoaji fomu za uteuzi katika majimbo hayo na kata hizo sita utakuwa ni
kati ya tarehe 12 hadi 18 Desemba, 2017 wakati katika jimbo la Songea
Mjini utoaji fumo utakuwa kati ya tarehe 14 hadi 20 Desemba, 2017.
“Uteuzi
wa wagombea katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata za
Keza, Kimandolu, Kwagunda, Bukumbi, Kurui na Kihesa utafanyika tarehe 18
Desemba, 2017 na uteuzi wa wagombea katika jimbo la Songea Mjini
utafanyika tarehe 20 Desemba, 2017” alisema Jaji Mst. Hamid.
Alifafanua
kuwa kwa upande wa kampeni za uchaguzi huo katika majimbo ya Singida
Kaskazini na Longido na kata zote sita zitaanza tarehe 19 Desemba, 2017
na kumalizika tarehe 12 Januari, 2018.
Katika
jimbo la Songea Mjini, alisema kuwa kampeni za zitaanza tarehe 21
Desemba, 2017 na kumalizika tarehe 12 Januari, 2018 wakati siku ya
uchaguzi katika majimbo yote matatu na kata zote sita itakuwa tarehe 13
Januari, 2017.
Mhe.
Jaji Mst. Hamid alivikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi
wazingatie Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yote wakati
wa kipindi cha uchaguzi mdogo wa majimbo hayo na kata Sita.
EmoticonEmoticon