TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
DESEMBA 28, 2017
RELEASE NAMBA 438,439,440,441 NA 442
LIGI KUU BARA MZUNGUKO WA 12 KUENDELEA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL) mzunguko wa 12 katika msimu wa 2017/2018 inaendelea wikiendi hii baada ya
kusimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA huko Kenya na mechi za raundi
ya pili ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).
VPL ambayo wadhamini wenza ni Kituo
cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) na KCB - Benki inayotoa huduma zake kisasa,
itaanza kesho Ijumaa Desemba 29, 2017 kwa mchezo kati ya Azam FC na Stand
United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00
usiku.
Jumamosi Desemba 30, kutakuwa na
michezo mitatu - Lipuli na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Samora
mkoani Iringa kuanzia saa 8:00 mchana; Mtibwa Sugar na Majimaji ya Songea
katika dimba la Manungu, Turiani mkoani Morogoro ilihali Ndanda itaikaribisha
Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona - Mtwara. Mechi hizo mbili zitachezwa
kuanzia saa 10:00 jioni.
Jumapili, mabingwa watetezi wa VPL,
Young Africans watakuwa wageni wa Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza
kuanzia saa 10:00 jioni huku Njombe Mji FC na Singida United wakitangulia kwa
mchezo utakaoanza 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
VPL itakamilisha mechi za mzunguko wa
12 katika mechi zitakazopigwa mwakani, Januari mosi ambako Mbeya City
wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Mwadui
wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu
itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi
ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na
7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na
17, 2018.
TFF KURASIMISHA MASHINDANO YASIYO RASMI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
lipo kwenye mkakati madhubuti wa kuyarasimisha mashindano yasiyo rasmi ili
kuweza kutambuliwa.
Kumekuwa na upotoshaji unaofanywa kwa
makusudi kuwa Rais wa TFF Wallace Karia amefuta mashindano yote ya aina hiyo
taarifa ambazo sio sahihi alichokisema Rais Karia wakati akizungumza na
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ni kuwa TFF inaandaa kanuni ili
mashindano yote ya aina hiyo yachezwe kwa kukidhi vigezo katika utaratibu mzuri
na watapata vibali kupitia FA wilaya na mikoa baada ya kutimiza vigezo
vitakavyowekwa wakati yale yenye sura ya kitaifa yatapata kibali kutoka TFF.
Nia ya TFF ni njema yenye lengo ya
kuufanya Mpira wa Tanzania kuwa katika muelekeo mmoja wenye kufuata utaratibu
wenye tija na wenye kuchochea maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini.
WATANZANIA WAENDELEA KUJITOKEZA KUNUNUA TIKETI ZA FAINALI ZA
KOMBE LA DUNIA ZA RUSSIA.
Watanzania wameendelea kujitokeza
kununua tiketi za Kombe la Dunia zitakazochezwa mwakani nchini Russia.
Mpaka sasa kati ya tiketi 290
zilizotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) tiketi za Fainali
tayari zimemalizika zikiwa zimebakia tiketi za nusu fainali na hatua ya
makundi.
Hatua ya makundi ya fainali hizo za
Kombe la Dunia ndio yenye tiketi nyingi zaidi zikiwa zimetolewa tiketi 250.
Yeyote mwenye nia ya kununua tiketi
awasiliane na Idara ya mashindano ya TFF mwisho Januari 15, 2018.
KADI MAALUMU ZA KUINGILIA UWANJANI KWA WAANDISHI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) inaendelea kusisitiza utaratibu kwa Waandishi wa Habari za Michezo wa
namna ya kuingia kuripoti mechi za fainali za kombe la Dunia zitakazofanyika
Russia mwakani.
Mwandishi anayehitaji kuripoti fainali
hizo awasiliane moja kwa moja na Idara ya Habari na Mawasiliano TFF ili kuweza
kupata kadi hizo maalumu (Accreditation) ambazo zinapatikana kupitia link
maalumu inayosimamiwa na idara hiyo.
Mwisho wa kuomba kadi hizo maalumu kwa
waandishi ili kuweza kuthibitishwa FIFA ni Januari 15, 2017.
TFF, OFISI YA MKUU WA MKOA KUWANOA MAKOCHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania TFF kesho anatarajia kuzindua rasmi kozi ya ukocha kwa Walimu wa Shule
za Msingi na Sekondari iliyoanza leo Desemba 28, 2017.
Kozi hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano
wa TFF na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam itakayochukuwa muda wa siku 10
itafanyika kwenye vituo viwili vya Makao Makuu ya TFF, Karume – Ilala na
Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
……………………………………………………………………..…… ………..……
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA