Kamati ya utawala ya shindano la tuzo
za utekelezaji maendeleo kwa kasi ya juu kwa Wabunge na Mawaziri (THSDA)
imezindua shindano la kutoa tuzo kwa Wabunge na Mawaziri watakaofanya
vizuri katika kutekeleza majukumu ya kuwaletea Wananchi maendeleo.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na
Katibu wa Kamati hiyo Bw. Wilson Maage alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari, juu ya uzinduzi wa shindano hilo ambalo litafanyika
kwa muda wa miezi miwili.
“Tuzo hizo zimetokana na kuwepo
wazo bunifu (intellectual property) ambalo azma yake ni kuhamasisha
utekelezaji wa shughuli za huduma na maendeleo kwa wananchi wa Tanzania
na kupima kasi ya utekelezaji wa shughuli hizo kwa viongozi wa ngazi
mbalimbali katika sekta na taasisi za kiserikali hapa nchini,” alifafanua Maage.
Aliendelea kusema kuwa, vigezo
vitakavyotumiwa katika kuteua viongozi hao ambao ni wabunge pamoja na
Mawaziri ni pamoja na kuwa mtetezi wa Wananchi wake bila uoga akiwa
ndani au nje ya Bunge, mtendaji bora wa maendeleo yenye kuonekana, sifa
ya kutoa hoja zenye tija kwa kutumia lugha ya staha bila matusi, sifa ya
utekelezaji wa haraka apatapo matatizo ya Wananchi wake pamoja na sifa
ya kutetea demokrasia, uhuru na kutetea wanyonge.
“Faida za shindano la tuzo hizi ni
kwamba zinaweka Wananchi karibu na viongozi, kuchochea utekelezaji
huduma na maendeleo kwa kasi ya juu, utawla bora na uwajibikaji wa
viongozi kwa Wananchi, uhusiano mzuri kati ya serikali na Wananchi na
kuimarisha furaha, utulivu na amani,” alieleza Maage.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa
Kamati hiyo, Herman Mnenuka alisema kuwa Wananchi ndiyo nguzo kuu ya
kupata kiongozi atakayepata tuzo hiyo kwani wao ndio watakaopendekeza
majina ya wabunge pamoja na wamaziri wanaofaa kuwania tuzo hiyo.
Katika tuzo hiyo, hatua ya kwanza,
wananchi wanapaswa kupendekeza wabumge 15 kwa kila kigezo shindanishi,
pia Wananchi watawateua Mawaziri 5 kwa kila kipengele shindanishi
kwaajili ya kuingia kwenye ushindani wa tuzo hiyo na wabunge watano na
Mawaziri watatu watakaopata kura nyingi kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS)
kutoka kwa wananchi wataingia katika fainali ya king’anyiro kuwania tuzo
hiyo.
Aidha aliongeza kuwa, katika hatua
nyingine, wananchi kupitia simu watawachuja washiriki waliofika hatua ya
fainali kwa kutuma SMS na mbunge pamoja na waziri atakayepata kura
nyingi ndiye atakaye kuwa mshindi katika kilele cha tuzo hiyo
kitakachofanyika tarehe 23 Desemba Mwaka huu.
“Niwaombe wananchi washiriki
kikamilifu ili kuweza kupata kiongozi anayejishughulisha na anayechapa
kazi kupitia tuzo hii na mwisho wa kilele tutapata mshindi wa kila
kipengele kilichowekwa ambacho kina tija muhimu katika taifa kupitia
waheshimiwa wabunge na mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alieleza Mnenuka.
Aidha aliongeza kuwa, Wananchi
watapendekeza majina kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu kupitia namba 15555
kwa mitandao ya Tigo, Airtel, Vodacom, Halotel Smart na Zantel na kila
SMS itatozwa gharama ya shilingi 500 vilevile kutakuwa na vipindi vya
radio runinga na magazeti ili kuwakumbusha mwenendo na hatua za shindano
la tuzo za THSDA hadi siku ya kilele.
Hizi ni tuzo za kwanza kuandaliwa hapa nchini na kamati hiyo ambazo zitafanyika kwa awamu
kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
EmoticonEmoticon