📌Serikali imewekeza zaidi ya bilioni 13 elimu ya Sekondari Chamwino
📌Uboreshaji wa miundombinu shilingi bilioni 17.9 zimetumika
📌Vijiji vyote 47 Chamwino vimewashwa umeme
📌Asema Sekta ya Nishati ipo salama
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuing'arisha Chamwino kwa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa Jimbo hilo.
Hayo yamebainishwa leo Februari 02, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka 5, (2020 2025) iliyowasilishwa na Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi.
"Nimemsikiliza Mhe. Ndejembi akieleza kazi kubwa ambayo Serikali imeifanya hapa Chamwino, ni dhahiri kwamba Serikali ya CCM chini ya Uongozi wa Dkt. Samia imefanya kazi kubwa ya kuing'arisha Chamwino na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa Jimbo hili. Hongereni sana, " Amesema Mhe. Biteko
Aidha, amewataka kuendelea kuisimamia Serikali kuanzia ngazi ya chini ili kuendelea kuyagusa maisha ya wananchi kikamilifu na kutatua kero na changamoto walizonazo.
"Ni ukweli usiopingika kwamba Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana na ya kutukuka ya kuiletea nchi yetu maendeleo. Ninyi hapa Chamwino ni mashahidi wakubwa wa maendeleo yaliyofanywa na Serikali chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan," ameongeza Dkt. Biteko.
Vile vile, Serikali imewekeza zaidi ya bilioni 13 katika kugharimia elimu ya Sekondari tu katika Wilaya ya Chamwino.
"Tunashuhudia kuendelea kukamilika kwa ujenzi wa Shule hii ya Mkoa ya Sekondari ya ya Bweni ya Wasichana Manchali ambapo Watanzania wote watapata huduma za elimu," ameongeza Dkt. Biteko
Katika hatua nyingine amesema kuwa, uboreshaji wa miundombinu kwa kujenga madaraja, vivuko na barabara za lami ndani ya Jimbo la Chamwino zaidi ya Shilingi bilioni 17.9 zimetumika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaj, Adam Kimbisa amewahimiza wakazi wa Chamwino kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao ili kulinda madanikio yaliyofikiwa.
Pia, amewata kutumiia mvua za msimu kulima kwa wingi na watakapopata mavuno wahifadhi sehemu ya mavuno yao ili kuwa na akiba ya chakula kwa siku zijazo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa jitihada za Rais Samia kutoa fedha za miradi zimechangia kuharakisha maendeleo ya jimbo ikiwemo usambazaji wa nishati ya umeme kwa wananchi.
"Kata zote 14 zenye vijiji 47 zimewashwa umeme ambapo kazi hiyo imefanyika katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024," amesema Mhe. Ndejembi.
EmoticonEmoticon