Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Filip Mpango akisoma maelezo ya mzigo huo ambayo
yalikuwa tofauti kabisa na uhalisia mara baada ya kuhakikiwa na timu ya Wataalamu wa Kitanzania wazalendo.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Filip Mpango (katikati) akiwa na viongozi wengine wa
Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) Biswalo Mganga (kushoto), Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA Charles
Kichere(kulia) wakiangalia Mzigo wa Almasi uliokamatwa katika uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Mzigo
huuo wa Almasi uliokamatwa katika uwanja wa Ndege ambao thamani yake ni zaidi
ya Tsh. Bilioni 64.
|
Dare es
Salaam, 09 Septemba, 2017: Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb), ameviagiza vyombo vinavyohusika kuchukua hatua za kisheria dhidi
ya kampuni ya Williamson Diamond Ltd na wote waliohusika kuidhinisha
usafirishaji wa madini ya almasi kutoka migodi ya kampuni hiyo na kudanganya
thamani halisi ya madini hayo kwa lengo la kuisababishia hasara Serikali.
Dkt.
Mpango ametoa agizo hilo leo tarehe 09 Septemba, 2017 baada ya kukagua madini
ya almasi yaliyokamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam yakisafirishwa kupelekwa nchini Ubelgiji.
Miongoni
mwa hatua za kisheria ni pamoja na kutaifisha madini yote ya almasi
yaliyokamatwa baada ya kubainika udanganyifu wa thamani yake halisi, kuwakamata
na kuwachunguza wote waliohusika katika udanganyifu huo wakiwemo wajumbe wa
bodi zilizomaliza muda wake na wafanyakazi waliopo na waliostaafu.
Almasi
hiyo ilikamatwa tarehe 31 Agosti, 2017 muda mfupi kabla ya kupakizwa kwenye
ndege ili isafirishwe kwenda nchini Ubelgiji, na ilipochunguzwa ilibainika kuwa
nyaraka za kampuni ya Williamson Diamond Ltd zimeonesha kuwa almasi hiyo ina
thamani ya Dola za Marekani Milioni 14.798 sawa na Shilingi Bilioni 33 za
Tanzania wakati thamani yake halisi ni Dola za Marekani Milioni 29.5 sawa na
Shilingi Bilioni 65 za Tanzania.
Kabla
ya kukagua almasi hiyo Waziri Mpango amepokea taarifa ya timu ya wataalamu
iliyofanya tathmini ya thamani halisi ya madini hayo ambapo kiongozi wa timu
hiyo Prof. Abdulkarim Mruma amesema pamoja na kubaini upotevu mkubwa wa fedha,
kuna dosari nyingine zikiwemo kukosekana kwa vifaa ya kupimia madini hayo,
almasi kusafirishwa na kuuzwa sokoni bila uwepo wa mwakilishi wa Serikali na
ameshauri hatua za udhibiti huo zifanyike katika madini yote yanayochimbwa hapa
nchini.
Pamoja
na kuipongeza timu iliyofanya tathmini hiyo na vyombo vya dola vilivyokamata
madini hayo Waziri Mpango amesema Serikali itatekeleza ushauri wote uliotolewa
na timu ya Prof. Mruma na kwamba kuanzia sasa almasi inayozalishwa hapa nchini
itasindikizwa na maafisa wa Serikali hadi sokoni na inataka kuanza kupokea
gawio halali kutoka mgodi huo.
Waziri
Mpango ametoa maagizo hayo mbele ya viongozi wa vyombo mbalimbli wakiwemo
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere,
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Biswalo Mganga, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John
Julius Mbungo, Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka na
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP - Lazaro Mambosasa.
Benny Mwaipaja
MKUU WA KITENGO CHA
MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
EmoticonEmoticon