DK.
NDUMBARO, MGONGOLWA WATEULIWA TFF
Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imeteua Kamati ya Rufaa ya Leseni za
Klabu, ikiwa ni maandalizi ya kuanza msimu mpya wa mashindano ya soka
yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.
Viongozi na wajumbe waliteuliwa
na kupitishwa Jumapili Julai 30, 2017 katika Mkutano wa Kamati ya Utendaji
uliofanyika Ukumbi wa Hosteli za TFF, zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume,
Ilala jijini Dar es Salaam yaliko Makao Makuu ya shirikisho.
Viongozi na Wajumbe
walioteuliwa ni Msomi Wakili Dk. Damas Ndumbaro atayekuwa Mwenyekiti; Msomi
Wakili Alex Mngongolwa (Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo) wakati Wajumbe ni
Meneja wa zamani wa Uwanja wa Taifa, Charles Matoke, Tumainiel Mlango na Ahmed
Menye.
Viongozi wa Kamati hiyo
watakuwa na majukumu ya kusililiza rufaa kutokana na uamuzi wa Kamati ya Leseni
za Klabu inayoongozwa na Msomi Wakili Lloyd Nchunga ambayo inasimamia
utekelezaji wa Kanuni ya 11 ya Ligi Kuu.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo ya
11, Klabu za Ligi Kuu zinawajibika na kutakiwa kuwasilisha maombi ya kupatiwa
Leseni ya Klabu kwa TFF katika muda utakaotangazwa na Kamati ya Utendaji ya TFF
na kuhakikisha zinakidhi masharti na vigezo vyote vya msingi kupatiwa leseni
ili kuweza kushiriki Ligi Kuu.
Kanuni hiyo ya 11 inasema
kwamba Klabu itakayoshindwa kukidhi kiasi cha kukosa Leseni haitashiriki Ligi
Kuu kwa msimu husika. Vigezo hitajika kwenye kupata leseni ya klabu ni kuwa na
Uwanja wa nyumbani wa mechi, uwanja wa mazoezi, umiliki wa klabu moja, kuwa na
timu ya vijana, uwepo wa ofisi rasmi na watendaji wake akiwamo mtendaji mkuu
(CEO) na maofisa masoko, habari na mhasibu mwenye taaluma ya uhasibu.
Tayari Klabu zilielekezwa
kuwasiliana na Meneja wa Leseni za Klabu, Jemedari Said ambaye ni Ofisa
Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania wa TFF kwa ajili ya maelezo ya kuchukua na
kurejesha fomu kwa mujibu wa taratibu na kanuni za mashindano kabla ya kuanza
rasmi mashindano.
LIGI
DARAJA LA KWANZA TANZANIA BARA 2017/18
Ligi Daraja la Kwanza Tanzania
Bara inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu kwa timu 24 zilizogawanywa
katika makundi matatu yenye timu nane kila kundi.
Tayari TFF, ilikwisha kutangaza
makundi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa timu 24 zitakazochuana msimu huu wa
2017/18 kuwania nafasi tatu muhimu za kupanda daraja kucheza Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2018/19.
Kwa mujibu wa makundi hayo
yaliyoratibiwa na Bodi ya Ligi ya TFF, kundi ‘A’ litakuwa na timu za African
Lyon, Ashati United, Friends Rangers za Dar es Salaam, JKT Ruvu na Kiluvya
United za Pwani, Mgambo JKT ya Tanga, Mvuvumwa ya Kigoma na Polisi Moro ya
Morogoro.
Kundi ‘B’ zitakuwa timu za
itakuwa na timu za Coastal Union ya Tanga; JKT Mlale ya Ruvuma; KMC ya Dar es
Salam, Mawezi Market ya Morogoro, Mbeya Kwanza ya Mbeya, Mufundi United ya
Iringa, Mshikamano na Polisi Dar za Dar es Salaam.
Kundi ‘C’ ina timu za Alliance
School, Pamba na Toto African za Mwanza, Rihno Rangers ya Tabora, Polisi Mara ya Mara, Polisi Dodoma ya
Dodoma, Transit Camp ya Shinyanga na JKT Oljoro ya Arusha.
Kadhalika, TFF imeagiza timu za
Ashanti United, Friends Rangers, KMC na Polisi Dar ya Dar es Salaam kuwasilisha
majina ya viwanja vitakavyotumiwa na timu zao wakati wa ligi hiyo inayotarajiwa
kuanza baadaye mwezi ujao.
Kutaja viwanja hivyo ni matakwa
ya Kanuni ya 6 (1) za kanuni Mama ya VPL inayozungumzia Viwanja kadhalika
kusomwa pamoja na Kanuni ya 11 inayozungumzia Leseni za Klabu kwamba kila timu
haina budi kuwa na viwanja vya mcehi za nyumbani ikiwa ni masharti ya kupata
leseni ya klabu.
SEMINA
YA MADAKTARI WA TIMU ZA LIGI KUU BARA
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), imeita semina ya siku moja kwa Madaktari wa timu za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara itakayofanyika Ijumaa Agosti 4, mwaka huu kuanzia saa 2.00
asubuhi kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya
Ligi Kuu, kila klabu ya Ligi Kuu inatakiwa kuwa na daktari wa timu ambaye
pamoja na mambo mengine atahakiki afya za wachezaji na viongozi wa timu.
Kila klabu inatakiwa
kuhakikisha daktari wake anahudhuria semina hii muhimu itakayoendeshwa na
Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya
Mwenyekiti wake Dkt. Paul Marealle.
Bodi ya Ligi itagharamia nauli
ya basi ya kuja na kurudi Dar es Salaam kwa kila mshiriki. Tunawatakia kila la
kheri katika maandalizi ya ushiriki wa semina hiyo ambayo ni sehemu ya
maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2017/2018.
UCHAGUZI
MKUU TAFCA AGOSTI 10, 2017
Uchahuzi Mkuu wa Chama cha
Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA utafanyika Agosti 10, mwaka huu mjini
Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi), Ramadhani Mambosasa ametangaza orodha ya majina sita ya mwisho ya
wagombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu Mambosasa, wagombea
hao kwa sasa hawana budi kuendelea na kampeni hadi Agosti 9, mwaka huu.
Waliopitishwa katika orodha ya
mwisho kuwania nafasi mbalimbali za uongozi - ngazi ya taifa ni pamoja na Kidao
Wilfred, Lister Manyara, Michael Bundala, Dismas Haonga, Jamhuri Kihwelo,
George Komba, Samuel Moja na Maka Mwalwasi na Mohammed Tajdin.
Nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Wajumbe wa
Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
EmoticonEmoticon