Katibu wa NEC, Idara ya
Organazesheni CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima akisalimiana na
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, kichama, Ramadhan Abdallah
Ali “ Kichupa” mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Mkoa huo
zilizopo Dunga Wilaya ya Kati Unguja.
Katibu wa NEC, Idara ya
Organazesheni CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima akitoa nasaha kwa
viongozi wa CCM Mkoa na Wilaya za Kusini na Kati Kichama katika ziara ya
kiongozi huyo visiwani Zanzibar.
Baadhi ya viongozi na Watendaji wa
ngazi mbali mbali za Chama na jumuiya zake Mkoa wa kusini na Wilaya
zake kichama. ( PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR).
…………………………
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
kimewataka viongozi na watendaji wa zamani wa ngazi za matawi waliowania
tena nafasi za uongozi katika uchaguzi unaoendelea hivi sasa ndani ya
chama hicho kutoshiriki kwenye vikao vya kuchuja na kujadili fomu za
wagombea wa nafasi za uongozi.
Tahadhari hiyo imetolewa na Katibu
wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima katika
mwendelezo wa ziara yake huko Mkoa wa Kusini kichama Unguja, alisema
mtu aliyewania nafasi ya uongozi ndani ya chama hicho hana haki ya
kujadili na kuchuja fomu za wagombea wenzake kwani kufanya hivyo ni
kinyume na Katiba ya Chama hicho.
Alisisitiza kwamba katika zoezi
hilo ni lazima kila kiongozi asimamie taratibu za uchaguzi ili kuepuka
malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
“ Kuna baadhi ya matawi kumetokea
changamoto za baadhi ya wagombea kujadili na kupitisha fomu za wagombea
wenzao jambo ambalo ni kinyume na taratibu za Kikatiba hivyo hatuwezi
kuvumilia vitendo hivyo ni bora uchaguzi urejewe katika maeneo
yaliyoripotiwa ukiukaji wa miongozo yetu”, alisema Nd. Pereira.
Nd. Silima alisema dhamira ya
chama hicho ni kuhakikisha chaguzi zote zitakazofanyika ndani ya chama
na jumuiya kuhakikisha wanapatikana viongozi bora waliopatikana kwa
mujibu wa matakwa ya Kikatiba na sio watu binafsi.
Katibu huyo aliweka wazi msimamo
wake kwamba atapambana vikali na baadhi ya watu waliopandikizwa katika
uchaguzi huo ili wapange safu na makundi ya viongozi wanaowataka wao kwa
baadhi ya ngazi za uongozi .
Aidha aliwasihi viongozi hao
kumpa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kiutendaji hasa
katika jukumu la kufanikisha uchaguzi unaoendelea na kuhakikisha
unakamilika kwa kiwango kilichokusudiwa.
“ Lengo la ziara yangu ni
kujitambulisha kwenu kwani toka nilipoteuliwa sijawahi kuja kwenu
kubadilishana mawazo pia naomba ushirikiano katika Idara yangu ya
organazesheni ambayo jukumu lake la msingi ni kusimamia shughuli zote
za chaguzi za chama na dola pamoja na masuala ya takwimu za wanachama.”,
alisema Silima.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo
ya uchaguzi wa chama hicho kwa ngazi za Matawi, Kaimu Katibu wa Wilaya
ya Kusini Kichama Unguja, Hafidh Hassan Mkadam alieleza kuwa
changamoto iliyojitokeza katika zoezi hilo ni baadhi ya Viongozi wa
ngazi husika kufanya uteuzi bila ya kuzingatia kanuni ya uchaguzi na
katiba ya CCM, hali iliyopelekea baadhi ya matawi kurejea zozezi hilo.
EmoticonEmoticon