Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa
Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, amewaasa wafanyakazi kuacha kufanya
kazi kwa mazoea na badala yake wajitume ili kuhakikisha dhamira ya
serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda inafanikiwa.
Alisema wakati
serikali inatekeleza kwa vitendo ujenzi wa viwanda katika maeneo
mbalimbali ya mkoa huo haina budi kila mmoja akachapakazi kwa bidii.
Alitoa rai hiyo
,wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa serikali na sekta binafsi
kwenye viwanja vya shule ya msingi Majengo wilayani Bagamoyo.
Mhandisi Ndikilo, alieleza mtumishi wa kila sekta mkoani humo anapaswa kuwajibika kikamilifu ili kuongeza maendeleo.
Alisema kuhusu
maslahi ya wafanyakazi, serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri
yatakayosababisha watumishi wa umma na sekta binafsi kuwa na morali ya
kujituma.
Aidha mhandisi
Ndikilo alisema, wakati serikali ikitekeleza azma ya ujenzi wa viwanda
jamii iendeleze watoto wao kielimu kwa lengo la kupata ajira baadae.
Nae Katibu wa TUICO
mkoani hapo, Kassim Matewele, alieleza pamoja na jitihada za serikali za
kutatua kero za wafanyakazi lakini bado wa sekta binafsi wanakabiliwa
na tatizo la kufanyakazi bila mikataba.
Alisema jambo hilo linawanyima haki zao kama wafanyakazi na kushindwa kuwekewa akiba zao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kwa mujibu wa
Matewele, hali hiyo pia inasababisha serikali kupoteza kodi ambayo
ingeweza kuingizwa kupitia pato la wafanyakazi hao.
EmoticonEmoticon