WIZARA YAKEMEA UBAKAJI WA MTOTO MKOANI IRINGA

March 15, 2017
JUKIII
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakemea vikali tukio la kubakwa kwa binti wa miaka saba  (jina limehifadhiwa) mkazi wa kata ay Kitanzini, mwanafuzi wa darasa la awali shule ya SUN Academy iliyoko kata ya Kwakilosa, manispaa ya Iringa.
Wizara imesikitishwa na taarifa za awali kuwa mtoto alibakwa katika mazingira ya shule mahali ambapo tunategemea pawe salama kwa mtoto kuishi. Wakati wote Serikali imekuwa ikisisitiza walezi wa watoto kuhakikisha wanalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ubakaji kwani vitendo hivi vimekuwa vikitaarifiwa kuwahusisha watu wa karibu wanaomzunguka mtoto katika familia, shuleni na jamii.
Wizara inapongeza vyombo vya habari vyote vinavyoibua matukio ya ukatili, kwa kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao utekelezaji wake unahusisha wadau wote nchini.
Wizara inamini kuwa Polisi kwa kutumia weledi na umahiri wao watashirikiana na wananchi, walezi, walimu na marafiki wa mtoto, kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanafichuliwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Wizara inawakumbusha wazazi na walezi kuwa vitendo vya ukatili ukiwemo ubakaji dhidi ya watoto wa kike havikubaliki katika nchi yetu kwani vitendo hivyo vinatia doa kubwa taifa letu. Natoa rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika kuwafichua waliohusika na ubakaji wa mtoto aliyeripotiwa kwa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Erasto T. Ching’oro
Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino Serikalini
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »