Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele
taarifa ya Tume aliyoiunda ya kuchunguza suala la Faru John, ofisini
kwake jijjini Dar es salaam Machi 27, 2017. (Picha na Ofisi ya `Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali , Profesa Samwel Manyele wakati
alipowasilisha taarifa ya tume ya uchunguzi wa suala Faru John baada ya
kukabidhi taarifa hiyo , Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam
Machi27, 2017.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kukabidhiwa taarifa ya tume
ya kuchunguza suala la Faru John na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa
Samwel Manyele, Ofisini kwake jijini Dar es salam Machi 27, 2017. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………..
*Ni ya uchunguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha Faru John kutoka kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele ambaye alikuwa akiongoza
tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amepokea taarifa
hiyo, leo (Jumatatu, Machi 27, 2017) kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya
Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo
cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga,
fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo
ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni
dume.
Prof. Manyele amesema matokeo
hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa katika hifadhi ya Sasakwa
Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.
“Maabara iliyotumika ni ya Chuo
Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya
wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa
matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea
yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya
kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake,” amesema.
Prof. Manyele amesema mapungufu
waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni kutokuwepo kwa kibali rasmi
cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru
John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo
ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Mengine ni uchukuaji holela wa
sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya
nchi; migongano ya kimaslahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia
taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na uwepo wa taasisi
nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Pamoja na kwamba mawasiliano
yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi
kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John
kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof. Manyele katika ripoti yake.
Akizungumzia kuhusu uchukuaji
holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha
nje ya nchi, Prof. Manyele amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya
sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri na kwamba tume inashauri TAWIRI
na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.
Amesema kuna umuhimu wa kudhibiti
watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu za vinasaba vya
wanyamapori (Genetic information) dhidi ya mataifa mengine. “TUME
inashauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe kitengo cha
Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA Forensic
Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake iweze kufanya maamuzi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa kimahakama katika kesi
za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru timu
ya uchunguzi iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi
iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu uliokuwemo ndani ya Wizara ya
Maliasili na Utalii na taasisi zake.
“Ofisi yangu itaipitia taarifa
hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo,
tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha Serikali imeamua kufanya nini juu
ya mapendekezo yaliyotolewa.”
Alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa
Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande,
afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na tume hiyo na wayafanyie kazi
mapema iwezekanavyo.
Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo
Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili za faru John na
taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha faru huyo. Hatua hiyo
ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha,
ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru
John kutoka kwenye hifadhi hiyo.
Alitoa agizo hilo alipotembelea
ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha
na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza
la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
EmoticonEmoticon