Waziri Mkuu wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa kulia akionyesha
taarifa ya Tume aliyounda kuchunguza kifo cha Faru John kutoka kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele jijini Dar es Salaam leo
………………………………………………………………………………………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Tume iliyoundwa kwa ajili ya
kuchunguza kifo cha Faru John imethibitisha kuwa Faru huyo alikufa
katika eneo la Sasakwa Grumeti kutokana na kukosa matunzo, uangalizi wa
karibu na matibabu alipoumwa.
Hayo yamesemwa leo Jijini, Dar es
Salaam na Mkemi Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele alipokuwa
akikabidhi ripoti ya uchunguzi wa Kifo cha Faru huyo kwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
“Sampuli zilizochukuliwa kwa
ajili ya uchunguzi wa vinasaba ni mifupa ambayo ilichukuliwa katika
mzoga wa Faru John uliokutwa eneo la Sasakwa Grumeti, Pembe
zilizochukuliwa hifadhi ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA), damu kutoka maabara ya NCAA na Chuo Kikuu cha Kilimo
Sokoine (SUA), ngozi kutoka kwenye mzoga na kinyesi kilichokaushwa
kutoka SUA,” alifafanua Prof. Manyele.
Aliendelea kwa kusema kuwa
matokeo ya uchunguzi wa awali yameonyesha damu, pembe, mifupa na ngozi
ni vya Faru John ambapo mpangilio wa vinasaba umeonyesho kuwa Faru huyo
ni mweusi (Black Rhinoceros) mwenye jinsia ya kiume.
Aidha vielelezo hivyo vilitumwa
Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini ambapo timu ya wataalam kutoka
Tanzania chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali walishiriki katika uchunguzi
wa awali wa vinasaba na kujadili matokeo kabla ya kuyatuma kwa Mkemia
Mkuu wa Serikali ambapo Matokeo yameonyesha sampuli na vielelezo vyote
ni vya mnyama pori Faru John.
Vile vile amesema, uchunguzi
umeonyesha kuwa sababu za kifo cha Faru huyo ni kukosa matunzo,
uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na
kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria pamoja na mapungufu ya kiuongozi
kwa Wizara, Hifadhi na Taasisi zake.
Baadhi ya mapungufu
yaliyobainishwa katika uchunguzi huo ni pamoja na kutokuwepo na kibali
rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru
John kutoka NCAA kwenda Grumeti.
Prof. Manyele amesema kuwa
hakukuwa na mkataba rasmi kati ya Serikali na mwekezaji unaoonyesha
mnyama ametoka Serikalini kwenda kwa Mwekezaji.
Tume hiyo imeishauri Serikali
kuchunguza viwanja vya ndege ndani ya hifadhi vinavyomilikiwa na
wawekezaji kutokana na kuwepo na uwezekano wa viwanja hivyo kuwa njia ya
majangili au matajiri kufanikiisha shughuli za ujangiri nchini.
Aidha kutokana na mapungufu ya
kiutendaji yaliyofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini
(kutokutoa kibali rasmi) na mapungufu ya kiuongozi yaliyofanywa na
Mhifadhi wa NCAA kuruhusu Faru John kuondolewa bila kibali, Tume
inashauri hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa ameipongeza timu hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Ameahidi kufanyia kazi maoni ya tume hiyo na kutolea maelezo ya hatua
zitakazochukuliwa na Serikali muda mfupi ujayo.
Tume ya uchunguzi ya kifo cha
Faru John iliundwa baada ya Waziri Mkuu kufanya ziara ya kikazi
Ngorongoro Disemba 6, 2016, ambapo alibaini kuhamishwa kinyemela kwa
faru huyo na kudaiwa kupelekwa Grumeti.
Waziri Mkuu alitaka ukweli kuhusu
upotevu wa Faru huyo na kuamua kuunda tume hiyo ili kubaini ukweli wa
Faru huyo kama alikufa au alitoroshwa.
EmoticonEmoticon