WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametembelea kiwanda cha kusindika samaki aina ya jodari na kuwakaribisha
viongozi wa kiwanda hicho kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa
viwanda vya samaki.
Amesema Serikali imeweka sera
nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya
uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo
aina mbalimbali za samaki.
Waziri Mkuu amesema hayo jana
jioni (Jumanne, Machi 21,2017) wakati alipotembelea kiwanda cha samaki
cha Mer des Mascareignes kilichoko jijini Port Louis nchini Mauritius.
“Tanzania kuna fursa nyingi za
uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza kwenye
viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa yenye
samaki wa aina mbalimbali,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali
imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongeza
tija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji
waliotayari kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na
Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed
alisema Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi wa kina
kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki.
Dkt. Khalid alisema lengo la
uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na
kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.
Naye Meneja Mkuu wa kiwanda hicho,
Bw. Patrick Hill alisema wamefurahi na mualiko wa kuja Tanzania kwa
ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari kushirikiana
na Serikali.
Alisema kampuni yao
inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na
wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa
wakiwa ni bara la Ulaya.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alitembelea kiwanda kingine cha Chantier Naval Del`Ocean Indien
Limited (CNOI) ambacho kinatengeneza na kukarabati meli , boti na
pantoni na kujionea uwezo mkubwa walionao, ambapo Watanzania wanaweza
kuja kujifunza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MACHI 22, 2017.
EmoticonEmoticon