Mteja aliyenufaika Melikizedek |
Dar es Salaam, Machi 2017- Moja ya makampuni yanayoongoza kwa bima ndogo Tanzania ambayo inatumia teknolojia ya simu za mkononi katika kutoa huduma za bima ya afya inaleta mapinduzi katika sekta ya ndani ya bima kupitia TigoPesa.
Kampuni ya Tigo kwa kushirikiana na kampuni Milvik ziliingia katika makubaliano ya kutoa Huduma hii tangu mwaka jana kwa kutoa Huduma ya bima kwa simu za mkononi ijulikanayo kama Bima Mkononi ambayo inatoa bidhaa za kipekee na za hali ya juu kama vile,bima ya maisha, ugonjwa na ajali kwa wateja wanaotumia Huduma ya TigoPesa.
Ikiwa na wateja hai zaidi ya 200,000, BimaMkononi ni mfumo mpya wa bima kwa Watanzania wa kawaida ambayo inawawezesha kuwakinga dhidi ya matukio yasiyotarajiwa yanayoweza kuwa na athari kubwa kwa hali ya kifedha kama wasingekuwa wamejiunga na huduma au mpango huu wa bima.
Tayari BimaMkononi ishalipa fidia ya zaidi ya shilingi milioni 27 katika miezi sita iliyopita.
Hawa Ramadhani ambaye ni mama wa watoto watatu kutoka wilaya ya Kibaha, mkoa wa Pwani ni mmoja wa wanufaika wa BimaMkononi. Akieleza jinsi BimaMkononi ilivyobadilisha maisha yake alisema; “Nilikuwa nimelazwa katika Hospitali ya tumbi kwa siku 21 na baada ya kuruhusiwa kutoka, niliwasilisha taarifa za hospitali katika duka la Tigo la huduma kwa wateja na nilifurahi waliponiita baada ya siku tatu na kupokea kitita cha 840,000/-! Alisema kuwa aliambiwa bima imemfidia kwa kipindi alichokuwa amelazwa hospitalini.
“Kwa pesa hizo niliweza kulipia ada ya shule ya watoto iliyokuwa imebaki, pamoja na kukuza biashara yangu ndogo,” alisema na kuwashauri wale ambao hawajajiunga na mpango huu kufanya hivyo ili wavune faida.
Mwingine ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia cha St. John, Dar es Salaam Melikizedeki Nyalufujo ambaye ni mnufaika mwenye furaha wa BimaMkononi baada ya kupokea 86,000/- kufuatia kulazwa kwake hospitalini kwa siku mbili kutokana na jeraha alilolipata.
“Mara ya kwanza nilipoelezwa kuhusu BimaMkononi nilikuwa na wasiwasi lakini nilijiunga. Hata hivyo nilishawishika kujiunga baada ya kupokea fedha hizo ndipo nilithibitisha kwamba ilikuwa ni kweli. Ankara za hospitali ilikuwa ni 16,000/-; hivyo kwa fedha hii ya ziada niliweza kulipia gharama nyingine kama vile kujikimu chuoni, kununia vifaa vya masomo na kulipia baadhi ya madeni madogo ambayo nilikuwa nimekopa hapo awali. Naishukuru mno BimaMkononi,” alisema Nyalufujo kwa furaha.
Kwa mujibu wa Meneja wa Milvik Tanzania,Tom Chaplin huduma ya BimaMkononi imetengenezwa makusudi kutoa bidhaa za Bima kwa Watanzania wote ambao wanaihitaji ambao vinginevyo wasingeweza kumudu huduma hiyo.
“Mteja anaweza kwenda kujisajili hospitali yoyote kwa vile hatuweki kizuizi cha hospitali gani mteja anaweza kutumia- tutayafanyia kazi madai wanapotutumia taarifa sahihi (taarifa ya kuruhusiwa kutoka, taarifa ya madai ya hospitali, fomu ya madai ya bima iliyosainiwa). Kitambulisho cha mteja ni ni namba yake ya simu na anaweza kujisajili kwa kutumia namba *148*15#, huduma hii inafikia wateja kupitia simu za mkononi kusaidia kufikiwa kwa urahisi kadri inavyowezekana kwa wakazi wa mjini na vijijini. Bima Mkononi hadi sasa imekuwa na matokeo makubwa katika kusukuma mbele kujumuishwa kifedha ndani ya sekta isiyo rasmi kwa kuwawezesha Watanzania kuzifikia huduma za bima wanazozimudu kutoka ndani ya simu zao.”
Tom Chaplain alieleza kuwa huduma hiyo imetengenezwa mahsusi kwa kuwapatia watu wote bima za maisha, afya na huduma binafsi ya ajali ambazo zinaweza kuzisaidia familia zao kusimamia madhara ya kifedha ambayo yanaweza kusababishwa na matukio yasiyotarajiwa.
Mkuu wa Huduma za Kifedha kwa Simu wa Tigo, Ruan Swanapoel alisema kwamba ushirikiano huu wa Tigo na Milvik katika kutoa huduma hii ni moja ya mkakati wa Tigo katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali na kuendelea kuongoza katika kutoa huduma za kibunifu na zenye ubora wa hali ya juu kuwezesha BimaMkononi kupatikana kwa kutumia TigoPesa.
“Huduma hii imekuwa ni fursa kubwa kwa wateja wa Tigo kuifikia bima kwa urahisi kwa sababu BimaMkononi inalenga kuwapatia Watanzania njia mbadala wanayoimudu katika bima ya afya na maisha,” alisema Swanepoel.
Kujisajili kwa ujumla wanachokihitaji wateja kufanya ni kupiga *148*15# na kufuata maelekezo. Kudai piga namba: 0659071001 na tutakusaidia namna unavyoweza kufungua madai.
Mwisho
EmoticonEmoticon