Pikiniki zinazofanywa na watu mbalimbali katika fukwe zilizoko kwenye ukanda wa utalii visiwani Zanzibar, zinachangia uharibifu mkubwa wa mazingira unaotishia kuwakimbiza watalii.
Shughuli ya kusafisha mazingira iliyofanywa juzi katika eneo dogo kwenye ufukwe wa Muyuni ulioko Matemwe mkoa wa Kaskazini Unguja, ilikusanya karibu tani moja ya takataka zikiwemo chupa za plastiki.
Operesheni hiyo iliyochukua saa moja, ilijumuisha wafanyakazi wa Amber Resort na Best of Zanzibar, na kusafisha eneo linaoandaliwa kwa ajili ya mradi mkubwa wa kitalii utakaofanywa na kampuni ya Pennyroyal.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Meneja Mradi wa Amber Resort Murtaza Hassanali, alisema vijana wanaotembeza watalii (mapapasi) pamoja na wageni wanaofika hapo, huondoka wakiacha vitu vingi visivyofaa ambavyo hugeuka kuwa taka na sumu kwa viumbe wa baharini.
Aidha alieleza kuwa, pikiniki zinazofanywa na watu kutoka mjini na maeneo mengine hasa vijana, ni chanzo kikuu cha uharibifu wa fukwe hizo.
"Angalia ufukwe wote umejaa chupa za plastiki, karatasi za foili, mifuko na viatu visivyofaa na hakuna mtu anayejali kusafisha. Hii ni hatari sana kwa ustawi wa mazingira ya baharini," alisema.
Hata hivyo, alisema kampuni yake inakusudia kuubadilisha ufukwe huo kwa kusambaza vifaa vya kuwekea taka na kutoa elimu kwa wakaazi wa kijiji hicho juu ya umuhimu wa usafi wa mazingira.
Aidha alisema kwa kushirikiana na serikali ya wilaya kupitia ofisi ya halmashauri, wataandaa mabango ya matangazo yanayohimiza wananchi kuhifadhi fukwe na maeneo yote ya kijiji hicho na kuyaweka katika sehemu tafauti.
Kwa upande wake, Nahya Khamis Nassor, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) anayesomea elimu ya afya na mazingira, alisema inasikitisha kuona fukwe zinazotegemewa kuwa kivutio kwa watalii, zimekithiri uchafu bila uangalizi.
Alifahamisha kuwa, Kamisheni ya Utalii Zanzibar inafanya kazi kubwa ya kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini kwa kusambaza vipeperushi vinavyoonesha uzuri wa mandhari pamoja na taarifa mbalimbali ili kuwashawishi watalii kuendelea kuja visiwani humu.
Hata hivyo, alisema pale watakapokuja na kukuta hali ni tafauti, watalii hao watahisi wamedanganywa na huenda wakafikiria mara mbili kabla hawajaamua kuja tena au hata kuvitangaza visiwa hivi kwa wananchi wenzao.
"Uchafu huu unaozagaa ufukweni unaishia baharini kwa kusombwa na maji yanapojaa. Plastiki haziozi na samaki wanaweza kuzila bila kukusudia na hii ni hatari kwa rasilimali za baharini kutoweka," alieleza Nahya.
Pamoja na kuwaomba wakaazi wa kijiji hicho kuzilinda na kuzihifadhi fukwe zao, aliishauri serikali ya wilaya kuunda kanuni maalumu zitakazosaidia kudhibiti uchafu unaotishia kuwakimbiza watalii.
Alisema itakuwa vyema, kanuni hizo ziweke adhabu ikiwemo faini kwa mtu yeyote atakaepatikana akichafua mazingira kwa makusudi kama inavyofanyika katika nchi na miji mingine.
Ofisa mratibu wa kampuni ya Amber Resort Mohammed Issa Khatib, alisema mpango huo utakuwa endelevu ili kuhakikisha elimu ya usafi wa mazingira inawafikia wananchi wote kijijini hapo na watu wengine wanaokitembelea ambao alisema ndio wanaoacha athari kubwa ya uchafu.
Aliwaomba wavuvi na vijana wanaofanya biashara za kitalii ufukweni waache kutupa taka ovyo, kwani kufanya hivyo kunachafua mandhari na taswira ya Zanzibar nzima mbele ya macho ya watalii.
EmoticonEmoticon