Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akitoa
ufafanuzi wa muongozo wa ukusanyaji wa mapato kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa
Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo
MD Kayombo akisisitiza jambo
Na Mathias Canal, Dar es salaam
Maafisa Watendaji wa Kata 14, Watendaji wa Mitaa 91 pamoja na Wahasibu
wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wameonywa kutopokea Rushwa wala
hongo ya aina yoyote kutoka kwa wamiliki wa biashara mbalimbali katika
Manispaa hiyo kwani kufanya hivyo watadhoofisha ukusanyaji wa mapato ya
serikali kama ilivyokusudiwa.
Kauli ya onyo imetolewa na
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati akitoa
ufafanuzi wa muongozo wa ukusanyaji wa mapato na kutoa maelekezo ya
majukumu ya kazi kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa kwenye kikao cha
kazi kilichofanyika leo Jumamosi Machi 18, 2017 katika ukumbi wa Ofisi
za Manispaa hiyo ilipo Mtaa wa Kibamba CCM.
Kayombo ameeleza kuwa
kwa mtumishi yoyote wa Manispaa kwa ngazi yoyote atakayebainika
kujihusisha na ubadhilifu kwa kuchukua Rushwa kwa walipa kodi
atachukuliwa hatua Kali za kisheria kwa kuiibia serikali kwani kuihujumu
serikali kwa kuiibia mapato au kuzuia ukusanyaji wa mapato ni kosa kwa
mujibu wa taratibu na sheria.
"Nina amini kwamba mnaishi vizuri
na wananchi wenu kwahiyo mnawafahamu vizuri wafanyabiashara wanaokwepa
kulipa Kodi lakini hata walipaji wazuri hivyo jambo la ukusanyaji mapato
litakuwa jepesi sana kwenu kutokana na uzoefu mlionao" Aliongeza
Kayombo
Mkurugenzi huyo amewasisitiza Watendaji hao kusimamia
vyanzo vyote vya mapato ikiwemo Hotel Levy, Service Levy, Mabango
makubwa na madogo (Bill Board), Leseni za biashara na Vileo, Upimaji
afya kwa ngazi za Mitaa hususani katika Migahawa.
Hata hivyo
amewataka Watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano, Uaminifu, na
Weledi mkubwa kwani kufanya hivyo kutasababisha ukusanyaji mkubwa wa
Mapato kwa mwaka 2016/2017.
Kayombo Amewataka Watendaji wote
kukagua Maduka yote katika maeneo yao ya kazi ili kubaini Maduka
yasiyokuwa na leseni na Yale yenye leseni kuwa na Leseni za Manispaa ya
Ubungo kwani wafanyabiashara wa Maduka mengi wamekuwa na kisingizio cha
kukata leseni na Kodi mbalimbali katika Manispaa ya Kinondoni na kutaka
kulazimisha kuitumia leseni hiyo kama halali kwa Manispaa ya Ubungo.
Sambamba na hayo pia MD Kayombo amewataka Maafisa biashara
kutochelewesha leseni za wafanyabishara waliokamilisha taratibu zote za
kumiliki leseni kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha huduma kwa wananchi
na kuongeza makwazo kwa wafanyabishara kwa sababu tu ya kuchelewa
kusaini leseni.
Alisema kuwa litakuwa ni jambo la aibu na
lisilovumiliwa kwa kuruhusu sheria zitungwe kwa umakini mkubwa lakini
utekelezaji wake uwe hafifu.
MD Kayombo aliongeza kwa kusema kuwa
hakuna Haki bila wajibu hivyo Watendaji hawapaswi kufanya kazi kwa
mazoea lakini pia kutofanya kazi kwa kuongozwa na tamaa.
MD
Kayombo amesema kuwa Oparesheni hiyo ya itakayodumu kwa miezi mitatu ya
ukusanyaji wa mapato itaanza jumatatu Machi 20, 2017 kwa ushirikiano
baina ya watendaji kutoka Makao makuu ya Wilaya, Watendaji wa Kata,
Watendaji wa Mitaa na wenyeviti wa serikali za Mitaa.
EmoticonEmoticon