Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba (katikati) akizungumza
na Waandishi wa habari juu ya Matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya
Serikali ya kusitisha uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya
pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba).
Mkutano huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa
Mazingira Bw. Richard Muyungi
Sehemu ya Waandishi wa habari
wakimsikiliza kwa makini Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba alipozungumza nao na kutoa
matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kusitisha uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa katika
vifungashio vya plastiki (viroba).
……………………………………………………………………………
Kama mnavyofahamu unywaji wa
pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki zimechangia
kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa nguvu kazi ya
taifa, ajali na vifo zivyosababishwa na unywaji uliokithiri wa pombe
hizi, kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na kupotea kwa mapato
yanayosababishwa na wafanyabiashara wasio waaminifu. Madhara haya ndiyo
yaliyopelekea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Majaliwa Kassim Majaliwa kutoa tamko tarehe 16 Februari, 2017 akiwa
Mererani, Mkoani Manyara kuhusu kusitisha uzalishaji, usambazaji,
uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya
plastiki (viroba) kuanzia tarehe 1 Machi 2017; Baadaye tarehe 20/2/2017
na tarehe 28/2/2017 nilitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu ufuatiliaji wa
agizo hilo.
Ili kutekeleza kwa ufanisi agizo
hili serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya kuratibu
Operesheni Maalum ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali na kuchukua
hatua stahiki.
Kikosi Kazi hicho kiko chini ya
uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, na kinajumuisha Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika
la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya
Ushindani wa Biashara (FCC), Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali (GCLA), Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi.
Operesheni maalum ya utekelezaji
wa maelekezo ya Serikali inaendelea kutekelezwa nchini kote kupitia
Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya pamoja na Kamati za
Mazingira za Mikoa na Wilaya. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa
zinawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya
operesheni hiyo Ofisi ya Makamu wa Rais. Majumuisho ya taarifa ya nchi
nzima yatafanywa baada ya Kikosi Kazi kuendesha Operesheni maalum katika
Jiji la Dar es Salaam kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 01 hadi 03
Machi 2017. Operesheni hii inatokana na kuwepo kwa Viwanda vingi na
wasambazaji wengi wa Pombe kali aina mbalimbali zilizofungashwa katika
vifungashio vya plastiki (sachets).
Ofisi ya Makamu wa Rais iliratibu
operesheni maalum katika Jiji la Dar es Salaam kwa siku tatu mfululizo
kuanzia tarehe 01 hadi 03 Machi 2017. Operesheni hii ilitokana na
kuwepo kwa viwanda vingi vinavyozalisha pombe kali za aina mbalimbali
zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki (sachets) ambazo
hazikidhi vigezo mbalimbali vya Sheria.
Kikosi Kazi maalum katika Operesheni hii tulikielekeza kufanya yafuatayo:-
- Kukagua na kuzuia (seize) pombe kali zilizofungashwa katika viroba (sachets) kwenye viwanda na kuorodhesha idadi ya pombe za viroba zilizopo, vifungashio (packaging materials), mitambo mahususi kwa ajili ya kufungashia pombe za viroba na mitambo ya kutengeneza vifungashio;
- Kukagua na kuzuia pombe kali zilizofungashwa katika viroba (sachets) kwenye maghala (warehouse /store), na maduka ya jumla (whole sale) na kuorodhesha idadi ya pombe kali zilizofungashwa katika viroba na vifungashio (packaging materials) tupu vilivyopo;
- Kubaini iwapo kuna mapungufu yoyote kwenye ufungashaji pombe kali;
- Kukagua viwanda vya kutengeneza vifungashio vya sachets kubaini kama kuna ukiukwaji wa Sheria;
- Kukagua uhalali wa vibali na nyaraka za uzalishaji / uendeshaji wa kiwanda / msambazaji husika (mfano vibali na vyeti vya TFDA na TBS, EIA, stempu za kodi za TRA, leseni za biashara, leseni za vileo);
- Kukagua nyaraka zinazoonesha kumbukumbu za uzalishaji na nyaraka za usambazaji (sehemu bidhaa zilipouzwa kwa jumla) ili kujua kama uzalishaji na usambazaji unafanyika;
- Kufanya tathmini ya Operesheni, kuboresha mapungufu na kuandaa ripoti ya Operesheni; na
- Kuchukua hatua yeyote inayolenga kuboresha Operesheni na hali inayojitokeza
- UKAGUZI ULIVYOFANYIKA
Jumla ya wakaguzi 58 walishiriki
katika zoezi hili na kugawanywa katika timu tatu (3) kulingana na
mikoa ya kikodi ya TRA Dar es Salaam, ambayo ni Temeke, Kinondoni na
Ilala. Aidha, timu hizo pia zilijumuisha askari polisi na
wanahabari.Katika operesheni hii, TFDA na TBS waliainisha viwanda
vinavyozalisha pombe kali, na Manispaa ziliainisha maduka, maghala na
baa zinazofanya biashara ya pombe kali kinyume na sheria.
Sheria mbalimbali za udhibiti
ikiwa ni pamoja na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura, 219; Sheria
ya Viwango Namba 2 ya mwaka 2009, Sheria ya Vileo ya mwaka 1968
(ilirejewa mwaka 2012), Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura, 191 na
Kanuni ya Kukataza Uzalishaji, Uingizaji na Matumizi ya Vifungashio vya
Plastiki kufungia Pombe Kali, iliyochapishwa katika Gazette Serikali
Namba 76 ya mwaka 2017 zilitumiwa katika kutekeleza Operesheni hii.
- MATOKEO YA UKAGUZI
Jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha
pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala manne, baa tatu na kiwanda
kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio vya plastiki
vya kufungashia pombe kali (viroba) vilikaguliwa ambapo matokeo ya
ukaguzi ni kama ifuatavyo:-
- Jumla ya carton 99,171 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba) zimekamatwa Kati yake vyenye ujazo wa mililita 50 ni carton 69,045 na milita 100 ni carton 29,344 za milliita 90 ni 782 Aidha, chupa zenye ujazo wa mililita 100 ni 10,625. Thamani yake ni Tshs bilioni 10.83
- Chapa mbalimbali za pombe kali za virobakama vile Red Wine, Banjuka, Officer’s Cane Spirit, Flash Ginna Dragon zilikuwa hazikidhi viwango na zilikuwa hazijasajiliwa na TFDA hapa nchini
- Makampuni yote yaliyokamatwa hayana Vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA). Makampuni mengine yalikuwa hayajalipa kodi TRA na hayakuwa na cheti cha TFDA na wala cheti cha TBS.
- Makampuni mawili yalikutwa yanazalisha na kusafirisha mizigo usiku
- Viroba vyenye thamani ya jumla ya Tshs 235 millioni vimekutwa vimefichwa kwenye maghala ya duka la jumla chini ya jengo la ghorofa (handaki) Kariakoo.
- Baadhi yapombe kali aina mbalimbali zilizofungashwa katika viroba na chupahazikuwa na namba ya matoleo (batch numbers) na tarehe za uzalishaji kwenye lebo (label);
- Baadhi ya pombe kali zilizoonekana wakati wa ukaguzi wa viwanda, maghala, baa na maduka ya pombe kali hazikuwa na stickers sahihi za TRA na nyingine zilikuwa na stickers ambazo zilihisiwa na TRA kuwa bandia, na hivyo kuhitaji uhakiki zaidi;
- Viwanda saba (7) vilikutwa vinafanya marekebisho kutokana na kusimamishwa awali na TFDA kwa kosa la kutoweka kabisa namba za matoleo na tarehe ya kuzalishwa kwa bidhaa au kuweka taarifa husika katika bidhaa chache walizozalisha hadi hapo watakapokidhi masharti ya TFDA;
- Baadhi ya pombe kali kwenye baadhi ya viwanda, maghala, maduka na baa zilikuwa zimefungashwa kwenye chupa zenye ujazo wa chini ya mililita 200 ambavyo ni rahisi kubebeka kama viroba.
- HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na:-
- Bidhaa za pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki zenye ujazo mdogo zenye thamani ya takriban Tshs 10.8 billionizimekamatwa na kuzuiliwa (seized) katika store za viwanda, maduka ya jumla, baa na maghala ya wasambazaji;
- Idara ya Uhamiaji imeagizwa kushughulikia raia wa kigeni wasio na vibali vya kuishi nchini ambao walikutwa kwenye baadhi ya viwanda wakati wa ukaguzi;
- Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeelekezwa kuvifuatilia na kuvichukulia hatua viwanda vyote vilivyokaguliwa na kugundulika kufanya kazi bila kuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment) au Cheti cha Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Auditing);
- Mamlaka ya Mapato Tanzania imelekezwa kufuatilia na kuchukua hatua stahiki kwa viwanda na maghala yote yaliyoonekana kuwa na bidhaa zenye stickers za TRA zinazosadikika kuwa bandia.
- TFDA na TBS wameelekezwa kufuatilia kwa karibu usitishaji wa ufungashaji wa pombe kali katika mifuko ya plastiki (viroba) na na chupa za ujazo mdogo chini ya 200mls; na
- Bidhaa zote zilizokamatwa zitabaki hivyo hadi Serikali itakapoelekeza hatua ya baadae.
- HATUA ZINAZOFUATA
- Kuendelea na na Operesheni hii nchi nzima kwa kasi zaidi. Aidha, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa, Wilaya hadi ngazi ya Vijiji zihakikishe agizo hili linatekelezwa nchini kote. Wenye viti wa Mitaa na vijiji wahusike pia kwa kushirikiana na kamati hizi. Aidha, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa zinawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni Ofisi ya Makamu wa Rais kila mara kwa kufuata maelekezo yatakayotolewa.
- Kufungua kesi mahakamani dhidi ya wafanyabiashara waliokiuka katazo hili ili adhabu kali kutolewa
- Viroba vyote vilivyokamatwa pamoja na mizigo mingine itabaki chini ya ulinzi kwa sheria zilizotumika na mtu yeyote haruhusiwi kufanya chochote hadi maelekezo zaidi yatakapotolewa na serikali.
- Kwa walioomba muda wa nyongeza kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, maombi hayo yatashughulikiwa baada ya Operesheni ya kuondoa pombe kali ambazo zimezalishwa na zinauzwa kinyume cha Sheria.
- WITO
Operesheni ya utekelezaji wa
kuzuia uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali
zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki nchini ni endelevu na
ina lengo la kuimarisha afya ya jamii, kudhibiti ukusanyaji wa mapato na
hifadhi ya mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Katika kutimiza
azma ya operesheni natoa wito ufuatao: –
- Kila mwananchi ashiriki katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kubaini wanaokaidi agizo la Serikali la kuzuia uzalishaji, usambazaji na matumizi ya pombe kali zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki na katika ujazo mdogo. Zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa ya wanaohusika na tutahakikisha usiri wa hali ya juu;
- Kwa atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa mtu anayezalisha, anayeuza au kutumia stempu feki za TRA, atapata zawadi ya shilingi milioni moja;
- Mtu atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa mtu yoyote mwenye kiwanda/mtambo wa kuzalisha pombe za viroba ambao hautambuliki na Serikali au mwenye mtambo wa kutengeneza viroba au kuchapisha chapa za viroba kinyume na sheria, atapata zawadi ya shilingi milioni moja.
- Mtu yoyote atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa mtu yoyote mwenye ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba kinyume cha Sheria atapata zawadi ya shilingi laki 5.
- Mtu yoyote atakayetoa taarifa ya kuwezesha kukamatwa kwa mtu au watu wanaoingiza nchini pombe za viroba kutoka nje ya Tanzania kinyume na Sheria na utaratibu atapata zawadi ya shilingi laki 5.
- Mtu yoyote atakayetoa taarifa ya kuwezesha kukamatwa na kushtakiwa mtu yoyote anayehamisha au kusafirisha pombe za viroba kinyume na Sheria na maelekezo ya Serikali atapata zawadi ya shilingi laki 5.
Taarifa hizi zitolewe kwa njia ya
ujumbe mfupi (SMS) au Whatsapp au kwa kupiga simu kwenye simu nambari
0685 333 444 au kwa Afisa yoyote kwenye Operesheni hii.
- Wafanyabiasharana wananchi waliokuwa wanajihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na uingizaji wa pombe kali zinazofungashwa katika viroba wanatakiwa kutii maelekezo haya ya Serikali mara moja;
- Taasisi za TFDA, NEMC na TBS zinaelekezwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ili kufikia malengo yanayotarajiwa; na
- Serikali za Mitaa kupitia Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji / Mtaa na Kata washiriki katika kuwatambua na kutoa taarifa ya watu au kikundi cha watu wanaojihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizifungashwa katika viroba; n
- Kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokamatwa na watakaokutwa wameshindwa kulipa kodi wanalipa kodi stahiki mara moja.
January Makamba (Mb)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
5 Machi 2017
EmoticonEmoticon