Kulia Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Rais Profesa Faustin Kamuzora, akitoa Tamko la Siku ya Mazingira Afrika kwa
niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.
January Mkamba, Leo katika mkutano na waandishi wa Habari Mtaa wa Luthuli
Jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira wa Ofisi hiyo
Bw. Richard Muyungi.
Ndugu Wananchi,
Tarehe
3 Machi kila mwaka watanzania wote huungana na nchi nyingine za Afrika katika
kuadhimisha Siku ya Mazingira Afrika, ambayo huadhimishwa barani Afrika kila mwaka. Siku hii imetengwa kwa lengo la
kukumbuka umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira barani Afrika. Azimio la
kuadhimisha Siku hii lilipitishwa na kuamuliwa na Baraza la Mawaziri
wanaosimamia Mazingira wa nchi za Afrika kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika
Kusini Mwaka 2002. Siku hii iliamuliwa iwe kielelezo cha kukuza weledi kuhusu
kupambana na uharibifu wa mazingira pamoja na kuenea kwa hali ya jangwa Afrika.
Kuanzia wakati huo siku hii ilikuwa inaadhimishwa nchini Ethiopia kwenye makao
makuu ya Umoja wa Afrika.
Ndugu Wananchi,
Kikao
cha 12 cha Baraza la Mawaziri wa Mazingira (AMCEN) kiliamua kwamba maadhimisho
ya siku hii yawe yanafanyika kikanda. Hivyo kuanzia mwaka 2009 maadhimisho ya
siku ya Mazingira Afrika yalianza
kufanyika kikanda katika nchi za Afrika na ndipo, mwaka 2010 nchi yetu ikapata fursa
ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya yaliyofanyika
jijini Arusha.
Aidha,
Umoja wa Afrika kwa kutambua juhudi na kazi iliyofanywa na Prof. Wangari
Maathai kutokana na mchango wa mwanamke huyu katika
hifadhi ya mazingira na kuwezesha
wanawake katika usimamizi endelevu wa maliasili na mazingira kwa ujumla waliamua
tarehe 3 Machi kila mwaka iwe pia ni siku ya kumkumbuka yake iende sambamba na
maadhimisho ya siku ya Mazingira Afrika. Hivyo tangu mwaka 2012
maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yamekuwa yakienda sambamba na
maadhimisho ya Siku ya Wangari Maathai
ili kutambua mchango wake katika utunzaji wa Mazingira. Mwanamke huyu alipata
Tuzo ya heshima ya Nobel Laureate's green
legacy kutokana na juhudi alizofanya.
Ndugu Wananchi,
Tunapoadhimisha
siku hii tutafakari kwa kina changamoto mbalimbali zinazochangia uharibifu
mkubwa wa Mazingira. Changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi,
kuongezeka kwa hali ya jangwa na ukame, uchafuzi wa mazingira, ongezeko kubwa
la idadi ya watu, kuwepo kwa shughuli za kiuchumi zisizoendelevu ambazo husababisha
uharibifu wa mazingira. Hali hizo husababisha ongezeko la joto, ongezeko la
ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, ongezeko la magonjwa mbalimbali ya mlipuko,
upotevu wa bioanuai, uhaba wa chakula na hivyo kusababisha kuwepo kwa ongezeko
la umaskini kwa jamii.
Ndugu Wananchi,
Tunafahamu
kabisa hali ilivyo sasa katika maeneo mengi nchini kwamba majira ya mvua yamebadilika
na kusababisha ukame. Hivyo, inabidi tuhakikishe tunavilinda vyanzo vya maji
kwa gharama yoyote ile. Aidha, katika kuadhimisha maadhimisho haya, kila mmoja
awawajibike ipasavyo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa
na matumizi yasiyoendelevu ya bioanuai na rasilimali zake. Hivyo kila mtu afanye
shughuli za kiuchumi zisizoharibu mazingira ikiwa ni pamoja na kutumia nyenzo za uvuvi endelevu, kutumia
nishati jadidifu, majiko sanifu na banifu, nishati mbadala, kudhibiti uchafuzi,
kupunguza uzalishaji wa taka na kusimamia ukusanyaji wa taka ili kuhakikisha
miji yetu inakuwa safi.
Ndugu wananchi,
Natoa
wito kwa watanzania tuadhimishe Siku ya Mazingira ya Afrika kwa kuendeleza na
kusisitiza kampeni ya usafi katika maeneno yetu. Aidha, ninawagiza wananchi
wote kuanzia ngazi ya Kaya, Mitaa, vikiwemo vikundi vya watu binafsi kushiriki
kwenye shughuli za usafi ili kuhifadhi mazingira yetu. Nitumie fursa hii
kuwakumbusha viongozi kuanzia ngazi ya
kijiji hadi mkoa kutumia fursa hii kuhuisha Kamati za Mazingira ili ziweze kusimamia
shughuli za utunzaji mazingira katika maeneo yao. Aidha, mikoa, halmashauri za wilaya,
sekta zote, pamoja na taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wote kwa ujumla kushiriki katika
shughuli za hifadhi na usafi wa mazingira wakati wote.
Ndugu wananchi,
Katika
kuadhimisha siku hii, natoa wito pia kwa viongozi na watendaji katika ngazi
zote kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingirakwa kuzingatia
sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni zake.
Baada
ya kusema hayo, nawatakieni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yenye
ufanisi.
Asanteni kwa
kunisikiliza.
EmoticonEmoticon