Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. January Mamkamba. (MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya
uzalishaji, uingizaji , usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki
maarufu kama viroba vinavyotumika kufungashia pombe kali, alipozungumza na
waandishi wa habari Ofisini kwake Mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam Leo.
Katikati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. January Makamba. (MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya
uzalishaji, uingizaji , usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki
maarufu kama viroba vinavyotumika kufungashia pombe kali, kulia ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Profesa
Faustin Kamuzora na Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira, Waziri
Makamba alizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake mtaa wa Luthuli Jijini
Dare es Salaam Leo.
JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA
MAKAMU WA RAIS
TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU MPANGO WA UPIGAJI MARUFUKU UZALISHAJI, UINGIZAJI, USAMBAZAJI NA
MATUMIZI YA VIFUNGASHIO VYA PLASTIKI (VIROBA) VYA POMBE KALI NCHINI
Mtakumbuka tarehe 20 Februari 2017
Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa tamko la Serikali la utaratibu utakaotumika
kutekeleza agizo la kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali
zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba)kuanzia tarehe 1 Machi
2017. Utekelezaji wa katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f)
cha sheria hiyo, na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na
marekebisho yake ya mwaka 2012.
Napenda
kusisitiza na kuujulisha umma wa Tanzania kuwa utekelezaji wa maamuzi haya ya
Serikali kuhusu usitishaji uingizaji, uzalishaji, uuzaji na matumizi ya
vifungashio vya plastiki vya kufungia pombe kali utaanza rasmi tarehe 01 Machi,
2017, katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Operesheni ya kukagua utekelezaji wa
agizo la serikali la usitishaji utengenezaji, uuzaji na matumizi
ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki itaendeshwa nchini kote kuanzia tarehe 2 Machi
2017 kwa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika
ngazi ya Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa. Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha taarifa
za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mnamo
terehe 24 Februari 2017, kiliitishwa kikao cha Mawaziri na viongozi wa taasisi
za Serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hili. Katika kikao hicho,
Wizara na taasisi za Serikali zilipewa majukumu mbalimbali, kama ifuatavyo:
1.
Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi,
imeanzisha mfumo wa stempu za Kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa
uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki.
Aidha, Mamlaka itahakikisha kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa
malighafi ya pombe kali (ethanol) wamesajiliwa na kwamba mfumo wa ufuatiliaji
wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa. Wazalishaji na waingizaji wa malighafi
hiyo watawauzia wale tu ambao wamepewa kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa
kila baada ya miezi mitatu (3) ya kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja
waliouziwa ambao wamesajiliwa. Uuzaji wa malighafi kwa watengezaji wa pombe
kali ambao hawajasajiliwa itakuwa ni kosa la jinai kulingana na Sheria.
2.
Mkemia Mkuu wa
Serikali ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na majumbani, atasajili
makampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za viwandani na majumbani nchini
ikiwa ni pamoja na Ethanol. Msajili
atawajibika kutoa taarifa sahihi za majina ya makampuni na watu binafsi na taasisi
zinazohusika, kiasi kilichoingizwa na kimetumika, pamoja na madhumuni ya
matumizi.
3.
Kulingana na
sheria ya Leseni ya Vileo Na 28 ya Mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka
2012, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika operesheni hii
itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa yote
Tanzania bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya biashara ya pombe ya kawaida na
pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume na masharti ya leseni za vileo
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
4.
Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
katika operesheni hii watakukagua viwanda vyote vinavyojihusisha na uzalishaji
wa vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia pombe kali kama
vimekidhi viwango vya kitaifa
vilivyowekwa. Ukaguzi katika viwanda vya plastiki utachunguza kama kuna
mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya pombe kali. Mitambo
ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kama haitumiki kwa kuzalisha bidhaa
zingine katika kiwanda husika, mwenye kiwanda atalazimika kutoa ufafanuzi wa
hatima ya mitambo hiyo. Mitambo ya kuzalisha vifungashio
vya plastiki itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia
vifungashio vya plastiki itakamatwa na kutaifishwa na wahusika watashtakiwa.
5.
Wizara ya Afya
Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee, kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
na mabwana afya katika operesheni hii
watatoa elimu kwa umma na kukagua maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na
kusambaza vileo vya aina zote, na kushiriki kukamata vileo ambavyo vipo kinyume
cha sheria na kanuni.
6.
Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo, itasaidia
kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hili.
7.
Wizara ya
Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama, itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala ya inteligensia.
8.
Ofisi ya
Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wataratibu operesheni.
Kama
tangazo letu la tarehe 20/2/2017 lilivyoonesha muda wa nyongeza unaweza
kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia
kwenye teknolojia ya chupa, na kwamba watahitaji muda mchache kufanya hivyo, na
ambao watatimiza masharti kadhaa na kupata kibali maalum kabla ya tarehe
28/2/2017. Hadi sasa Serikali imepokea maombi ya wazalishaji 9. Tutangaza kesho
iwapo kuna ambao wamekidhi masharti au la. Kanuni za upigaji marufuku pombe
hizi zipo tayari.
Pia
tumepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi kwamba zoezi hili limekuja ghafla na
wengine wana malighafi na bidhaa kwenye maghala. Ukweli ni kwamba Serikali
ilitoa taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei 2016, na mara kadhaa baada ya hapo,
na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi. Vilevile, taarifa ya Serikali iliyotangaza
kupiga marufuku pombe za viroba ziliripotiwa kwa ukubwa stahiki kwenye vyombo
vya habari, ikiwemo kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwananchi, mwezi
Agosti 2016. Katika taarifa zote za nyuma, Serikali ilitangaza kwamba hatua
hiyo itaanza tarehe 1 Januari 2017. Hatua hizi zimechelewa kwa miezi miwili.
Iwapo, baada ya taarifa hizo za Serikali, kuna mzalishaji ameagiza malighafi au
kutengeneza au kuhifadhi pombe za viroba, au kuchukua mkopo kwa ajili hiyo,
atakuwa amefanya hivyo akijua madhara yake.
Mwisho napenda
kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji marufuku matumizi ya
pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) kwa kutoa
taarifa kwa vyombo husika ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze
kuchukuliwa hatua stahiki. Zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa
zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
28/02/2017
28/02/2017
EmoticonEmoticon