Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akimuhoji Kaimu Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika Masasi Mtwara
(MAMCU) Bwana Kelvin Rajabu kuhusiana na upotevu wa koroshozaidi ya tani
2000 Waziri mkuu alifanya kikao na Bodi ya korosho pamoja na baadhi ya
wanaushirika Mamcu kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano
Ikulu ndogo Mkoani Ruvuma
Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma
Zuberi Mwombeji akiwatarifu Maofisa wa Mamcu na Yurap wako chini ya
ulinzi wa polisi kuhusiana na upotevu wa korosho tani 2000 kulia mwenye
kaunda suti Kaimu meneja mamcu Bwana Kelvin Rajabu anayefuatia
Mkurugenzi wa YURAP inayojishughulisha nauhifadhi korosho katika Ghala
la BUCO Masasi Bwana Yusuf Namkula anayefuatia Mkurugenzi mwenzake Bwana
Ramadhan Nama na Meneja tawi la Mamcu Bwana Lawrence Njozi
Watuhumiwa wakipelekwa kupanda gari la polisi kwa ajili yakuwapeleka rumande
Kaimu Meneja wa Mamcu bwana Kelvin Rajabu akipanda gari la polisi tayari kwakwenda rumande
Picha na Chris Mfinanga
*Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000
* Wapelekwa Masasi chini ya ulinzi wakajibu tuhuma zinazowakabili
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa
Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha
wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani
2, 138 za korosho.
Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu
Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja
Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya
YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw.
Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.
Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo
kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana jioni (Jumamosi, Januari
7, 2017) baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU,
wamiliki wa ghala la BUCO – Masasi na kikundi cha wakulima sita
waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za
Mtwara na Masasi.
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu
alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za
korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonyesha kuwa
waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa
katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw.
Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa
na zilishalipwa an wanunuzi wa mnda wa tano lakini akadai hakupewa
taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala
la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo
ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani
zilipo.
“Tangu mnada wa tano,
mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama
kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima
hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa
yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila
kupata majibu ya kueleweka.
Tuhuma zinazowakabili maafisa hao
wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani,
wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote
juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa
chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.
Nyingine ni kutowalipa fedha kwa
wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10
Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza
korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.
Nyingine ni kutopelekwa mnadani
kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya
Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana; kutokutolewa taarifa ya
kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara
wananchi.
Tuhuma nyingine ni kushindwa
kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye
mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na
Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200);
Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).
Kutokana na mapungufu hayo, Waziri
Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi
ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi
cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za
MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa
ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.
Mapema, wakisoma risala yao kwa
Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero nyingi sana kama vile
kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo
walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali
ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa
MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.
“Makubaliano yalikuwa ni kwamba
mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini
hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini
hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa. Pia kuna makato
yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao wameyaacha na
unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia gharama za
unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye pia ni
mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.
Wakulima hao wa korosho kutoka
Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha
Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es Salaam ili
wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Mheshimiwa Rais Dk. John
Magufuli.
Kwa kutambua umbali uliopo kutoka
Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku
waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua kuwaita wakulima hao
wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JANUARI 8, 2017.
EmoticonEmoticon