Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, akimkabidhi kompyuta sita Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ado Mapunda kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ofisi za umma mkoani Mara. Wengine kwenye tukio hilo ni watumishi wa Bayport, akiwamo Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Bayport, Lugano Kasambala wa kwanza kushoto. Picha na Mpiga Picha Wetu Mara.
Na Mwandishi
Wetu, Mara
SERIKALI ya
Mkoa Mara kwa kupitia Katibu Tawala wake, Mheshimiwa Ado Mapunda, imewaagiza
watendaji wa serikali mkoani humo kuhakikisha kompyuta walizopewa na Taasisi ya
Kifedha ya Bayport Financial Services, zinaelekezwa kwenye shule za kata ili
kuchangia ukuzaji wa kiwango cha elimu.
Mheshimiwa
Mapunda aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati anapokea kompyuta sita kutoka Bayport
zilizoelekezwa katika Halmashauri ya Tarime, Rorya na Manispaa ya Musoma, huku
kila ofisi ikipata kompyuta mbili ikiwa ni mwendelezo wa ugawaji wa vitendea
kazi kutoka kwenye taasisi hiyo inayojihusisha na mikopo ya fedha taslimu kwa
watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni zilizoidhinishwa.
Akizungumza
katika makabidhiano hayo, Katibu Tawala huyo alisema lengo la Mkoa wao ni kuona
kiwango cha elimu kinapiga hatua kubwa, hivyo wameona msaada huo uelekezwe
zaidi katika shule za kata kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu muhimu za
wanafunzi wao.
Alisema
kufanya hivyo kutaongeza ukuzaji wa elimu ya wanafunzi wa mkoani Mara, ili iwe
njia ya kuandaa wataalamu wazuri kwa kutumia vema teknolojia ya kompyuta inayoboresha
utendaji wa kazi.
“Tunashukuru
wenzetu wa Bayport wa Kanda ya Ziwa pamoja na Makao Makuu kwa kutuletea msaada
huu mkubwa kwetu ambao kwa hakika tutautumia vizuri katika Mkoa huu wa Mara ili
ulete tija kama mlivyokusudia wakati mnafikiria kusambaza.
“Ofisi yetu
imeagiza kompyuta hizi zisambazwe katika baadhi ya shule za kata kwa kuzitumia
kwa namna moja ama nyingine ili wanafunzi wetu wasonge mbele zaidi kwa kuanzia
kurekodi vizuri takwimu zao kama njia ya kugundua tunafanya juhudi za kutuvusha
hatua ya juu zaidi,” Alisema Mapunda.
Naye Mratibu
wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa,
alisema ndoto zao zinaelekea kukamilika kuhakikisha kwamba msaada wa kompyuta
zao unafika kwa haraka kama walivyokusudia na kuuzindua mwaka jana jijini Dar
es Salaam.
“Kompyuta
tulizotoa Mara na Kanda ya Ziwa ni mwendelezo wetu wa kutoka kwenye kompyuta
125 tulizomkabidhi Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huku 80 zikielekezwa mikoani na kuufanya
mzigo wote ufikie 205 wenye thamani ya Sh Milioni 500,” Alisema Mercy.
Mbali na
Mara, Bayport pia walikabidhi kompyuta mbili kwa Halmashauri ya Wilaya
Misungwi, mkoani Mwanza na kuifanya Kanda ya Ziwa kuvuna kompyuta nane za
taasisi hiyo ambapo pia ilitangaza kuwa utaratibu huo wa kufikisha kompyuta utaendelea
katika wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara wakiamini utasaidia kuongeza
ufanisi katika ofisi za umma.
EmoticonEmoticon