AZAM FC YAANZA VYEMA MAPINDUZI CUP YAILAZA ZIMAMOTO SC

January 02, 2017
azam-vs-kagera-4
Timu ya Azam FC ya jijini Dar es salaam imeanza vyema michuano ya Mapinduzi Cup inayoendelea visiwani Zanzibar baada ya kuwanyuka wenyeji Zimamoto goli 1-0 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Amani na ukiwa mchezo wa kwanza wa Kundi B.
Kipindi cha kwanza hakuna aliyeweza kumtambia mwenzake baada ya kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa kutokana na timu hizo kucheza mchezo kwa kutegeana huku Zimamoto wakikosa nafasi nyingi za wazi.
Kipindi cha pili kilianza huku kila timu ikiamini kutoka na pointi tatu muhimu kutokana na kupewa maelezo toka kwa makocha wao na pia zikifanya mabadiliko ya kuongeza nguvu hata hivyo mabadiliko hayo yaliwasaidia Azam FC.
Akitokea benchi Mshambuliaji Kinda Shaaban Idd alifunga goli dakika ya 79 baada ya kumpiga kanzu mlinda mlango wa Zimamooto SC na kuiandika bao safi na kumnyanyua benchini kaimu kocha wa Azam FC Idd Nasor Cheche kwa furaha.
Dakika 87 Nyange Othumani aliinyima goli la wazi la kusawazisha Zimamoto baada ya kupokea safi huku akibaki yeye mwenyewe  Aishi Manula na kupiga shuti lake nje ya lango hadi mwamuzi anamaliza Mpira Azam Fc wameibuka na ushindi wa goli 1-0 na kuongoza kundi B.
Huu ni ushindi wa pili kwa kaimu kocha wa Azam FC Idd Nasor Cheche baada ya kupokea mikoba toka kwa Wahispania ambao walitimuliwa na mchezo wake wa kwanza ulikuwa wa Ligi Kuu Tanzania bara baina ya Tanzania Prisons ambapo Azam FC waliibuka na ushindi wa goli moja mfungaji akiwa ni John Bocco
Mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Visiwani humo ni ule wa usiku saa 2:30 ambapo bingwa Mtetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania bara Yanga watatupa karata yao ya kwanza kucheza na Jamhuri toka visiwani Pemba.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »