Waziri Mkuu Kassim Majiliwa
amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Molard Tanzania Bwana
Abeid Abdallah ambaye kampuni yake inajishughulisha na ujenzi wa nyumba
za kisasa kwa gharama nafuu Waziri mkuu ameikaribibisha kampuni hiyo
kujenga nyumba za watumishi Mkoani Dodoma mazungumzo hayo yamefanyika
ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya
Molard Bwana Abeid Abdallah akimuonyesha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
baadhi ya picha na michoro ya nyumba za kisasa na zabei nafuu zinazo
weza kujengwa Dodoma Picha na ofisi ya Waziri Mkuu
………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameikaribisha kampuni ya ujenzi ya Moladi Tanzania ielekeze nguvu zake
Dodoma ambako kuna mahitaji makubwa ya nyumba za watumishi.
“Natambua kuwa mnatumia
teknolojia ya kisasa na ujenzi wa nyumba zenu unachukua siku chache
sana. Ninawaencourage mje Dodoma ambako kuanzia Machi mwakani, watumishi
wengi wataanza kuhamia huko,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo
mchana (Jumatano, Oktoba 12, 2016) wakati akizungumza na Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah ambaye alifika ofisini
kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam na kumuonyesha ramani ya nyumba za
watumishi ambazo wanazitumia.
Waziri Mkuu amesema Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina maeneo ambayo imeyatenga rasmi
kwa ajili ya viwanja vya makazi na anaamini katika muda wa miezi miwili
wanaweza kujenga nyumba za kutosha watumishi wanaotarajiwa kuhamia
katika awamu ya pili.
“Nimeangalia michoro yenu, nyumba
za vyumba vitatu vya kulala zina hadhi ya kukaa hata wakurugenzi; na
watumishi wa kawaida wanaweza kumudu zile za vyumba viwili vya kulala…
ninawatia moyo mwende haraka Dodoma na wale ambao wako serious wataleta maombi yao mara moja,” amesema.
Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona kuwa size
ya ramani zao inatosha kwenye kiwanja cha ukubwa wa mita za mraba 550
ambacho ni high density na watumishi wengi wanaweza kumudu kuvinunua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo,
Bw. Abdalla amemweleza Waziri Mkuu kwamba nyumba ya ukubwa wa vyumba
vitatu vya kulala, yenye sebule, jiko, stoo na choo inatosha eneo la
mita za mraba 94 tu.
“Kati ya vyumba hivyo vitatu,
kimoja ni master, pia kuna sebule, chumba cha kulia na kibaraza. Hii
inaanzia shilingi milioni 35 hadi milioni 41 kutegemea na aina ya vifaa
unavyoweka kwenye umaliziaji. Lakini tukiongeza na servant quarter utalazimika kulipia shilingi milioni 7 ambapo unapata vyumba viwili na choo na bafu ndani,” amesema.
“Kimsingi, ni lazima tutaweka
madirisha, milango, vyoo, masinki ya bafuni na jikoni, tiles (na mtu
anaruhusiwa kuchagua za China, Italy au Spain),” ameongeza.
Akifafanua kuhusu nyumba yenye
vyumba viwili vya kulala, Bw. Abdalla amesema nayo pia ina sebule, jiko,
stoo na choo kimoja na inatosha eneo la mita za mraba 54. Amesema
nyumba hizo zinaanzia sh. milioni 20 hadi 25 kutegemeana na aina ya
vifaa vinavyowekwa kwenye umaliziaji.
Amesema ujenzi wa nyumba moja
unachukua wiki sita na kama viwanja viko eneo moja au jirani, wanaokoa
muda wa siku tatu hadi tano kwa kila nyumba. “Tunajenga ukuta kwa
kumwaga theluji isiyochanganywa na kokoto ambayo ni mchanganyiko wa
saruji, mchanga na kemikali. Inakauka baada ya saa saba na ukuta wetu ni
imara mara nne zaidi ya ukuta uliojengwa na tofali la zege.”
Teknolojia yetu inawezesha ukuta
wa nyumba nzima kukamilika ndani ya siku sita, nyumba zetu zinastahimili
matetemeko, vimbunga na ujenzi wake unapunguza gharama za ujenzi kwa
asilimia 40.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji
wa nyumba hizo, Bw. Abdalla amesema wana mikataba na mabenki kwa hiyo
wanaweza kujenga nyumba na kuziuza mara moja lakini pia wananchi
wanaweza kuingia mikataba na mabenki na kulipia kidogo kidogo katika
muda maalum (mortgage).