Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea hundi ya Shilingi milioni 16 kutoka kwa Dkt. Ave Maria
Semakafu (kulia), Berious Nyasebwa (wapili kushoto) na Benjamin Thomson
wote kutoka Group la Whats App la Leaders Forum ukiwa ni mchango wa
group hilo kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es
salaam Septemba 21, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwashukuru viongozi wa Jumuiya ya Ahmadiyya ambao walitoa mchango wa
shilingi milioni 10 kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera,
Septemba 22, 2016. Makabidhiano hayo yalifanyika ofisini kwa Waziri Mkuu
jijini .Kutoka kushoto ni Sheikh Tahir Mahmood Chaundhry, Issa
Mwakitalima, Khuram Shahzad na Jamil Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea mchango wa tani 40 za saruji zenye thamani ya shilingi milioni
16.5 kutoka kwa Dhruv Jog na Lebulu Victor (kulia) wote wa Kampuni ya
ujenzi a Advent ukiwa ni mchango kwa waahirika wa tetemeko la ardhi
mkoani Kagera Septemba 22, 2016. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini
kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea hundi ya shilingi milioni 100 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya VODACOM TANZANIA, Bw. Ian Ferrao (kulia) na Mkurugenzi Mkuu
wa Kampuni hiyo, Rosalynn Mworia ukiwa ni mchango kwa waarhirika wa
tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Ofisini kwake jijini Dar es salaam
Septemba 22, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Meneja wa Kanda wa
LAPF, Amina Kassim (kulia) na Kafiti Kafiti wa LAPF ukiwa ni mchango
wa Mfuko huo kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es
salaam Septemba 22, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea sehemu ya msaada ya vyakula wenye thamani ya shilingi milioni
10 kutoka kwa viongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Art of Living ukiwa ni
msaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Septemba 22,
2016. Kutoka kushoto ni Nishitha Kulshreshtha, Nishit Patel, Neha
Movaliya,Sharik Choughule ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Shina la
Pamba Road, Upanga na Neha Movaliaya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………..
TAASISI sita zikiwemo za dini na
kijamii zimechanga jumla ya sh. milioni 172.5 zikiwa ni misaada kwa
wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera
Septemba 10, mwaka huu.
Mchango huo umepokelea leo jioni
(Alhamisi, Septemba 22, 2016) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye
ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Bw. Ian Ferrao alisema kiasi cha sh.
Milioni 100 kimekusanywa kutoka kwenye mfuko wa Vodacom Foundation
pamoja na wadau wao.
Bw. Ferrao amesema kampuni ya
Vodacom imekuwa mstari wa mbele kusaidiana na Serikali katika uboreshaji
wa miradi mbalimbali za kijamii…..
Taasisi nyingine iliyochangia ni
Mfuko wa Pensheni wa LAPF ambapo Meneja wa Kaya ya Dar es Salaam, Amina
Kassim amemkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 20.
Pia Jumuiya ya Kiislam Ahmadiyya
imekabidhi msaada wa sh. milioni 10 kati ya hizo sh. milioni nne ni
fedha taslimu na zilizobaki ni mabati na mifuko ya saruji.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya
ujenzi ya Advent, Dhruv Jog amemkabidhi Waziri Mkuu msaada wa tani 40 za
saruji yenye thamani ya sh. milioni 16.5 na kusema kwamba wameshtushwa
na tukio hilo na tayari saruji hiyo imeanza kupelekwa Kagera.
Kwa upande wake mwakilishi wa
Taasisi ya kimataifa ya Art of Living, Neetu Kulshreshtha wametoa msaada
wa vyakula mbalimbali pamoja dawa vikiwa na thamani ya sh. milioni 10.
Dk. Ave Maria Semakafu
amemkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh milioni 16 kwa niaba ya makundi
mawili ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp. Makundi hayo yanaitwa Leaders
na Uongozi.
Akitoa shukrani kwa waliotoa
michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi
kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa
walengwa.
“Tunashukuru sana kwa michango
yote. Tunashukuru na makundi ya WhatsApp ya Leaders na Uongozi ambayo
nayo yameamua kuja kutuchangia. Michango hii inaonyesha kuguswa na
mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali
inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi
kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa
ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.
Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Tetemeko hilo lililotokea
Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na
wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya
Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38
wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji
mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha
nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi
baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi
126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
EmoticonEmoticon