Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akisalimiana na
sehemu ya watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na
wakandarasi wanaosimamia miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mara baada ya kuwasili wilayani Handeni
mkoani Tanga.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Mkuu wa Mkoa
wa Tanga, Martine Shigela (kushoto) wakifuatilia taarifa ya utekelezaji
wa miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na REA Awamu ya Pili (REA II)
iliyokuwa inasomwa na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
mkoani Tanga Mhandisi Abdulrahman Nyenye (hayupo pichani)
Meneja
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Tanga Mhandisi
Abdulrahman Nyenye akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme
vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mbele ya Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wengine
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Handeni, Wizara ya
Nishati na Madini, TANESCO na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA.
Mkuu
wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela akielezea mafanikio ya miradi ya
usambazaji wa umeme vijijini iliyotekelezwa na Wakala wa Nishati
Vijijini Awamu ya Pili (REA II).
Na Greyson Mwase, Tanga
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa serikali
imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 kila mwananchi
anapata umeme wa uhakika na kupelekea uchumi wa nchi kukua kwa kasi.
Profesa
Muhongo aliyasema hayo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa
miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa
Nishati Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kutoka kwa watendaji wa Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Tanga. Profesa Muhongo yupo mkoani
Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na
REA pamoja na kuzungumza na wananchi.
Profesa
Muhongo alisema kuwa kwa kutambua mchango wa nishati ya umeme katika
ukuaji wa viwanda nchini, serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa
kasi ya usambazaji wa umeme vijijini inaongezeka ili ifikapo mwaka 2020
mgawo wa umeme uwe ni historia
Alieleza
kuwa serikali imeamua kuweka nguvu katika usambazaji wa umeme hususan
katika maeneo ya vijijini ili kufuta umaskini kwani kupitia nishati ya
umeme wananchi waishio vijijini wana uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo
vidogo na kuongeza ajira na kupunguza wimbi la vijana wengi kukimbilia
mijini kwa ajili ya kutafuta maisha.
Akielezea
mpango wa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini itakayosimamiwa na
REA Awamu ya Tatu (REA III), Profesa Muhongo alisema kuwa serikali
imetenga zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme
katika maeneo yote kipaumbele kikiwa ni katika vijiji vilivyokosa umeme
REA Awamu ya Pili. (REA II) Hata hivyo Profesa Muhongo alieleza kuwa
wakandarasi waliokwamisha miradi ya REA Awamu ya Pili hawatapewa kazi ya
kusambaza umeme vijijini katika REA Awamu ya Tatu.
“Serikali
iko makini katika kuhakikisha kuwa wakandarasi wenye sifa wanapewa kasi
ya kusambaza umeme vijijini, hatuhitaji wakandarasi wasiotekeleza
miradi kwa wakati,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo aliwataka wakandarasi wa kitanzania wenye vigezo kujitokeza na
kuchangamkia fursa ya kusambaza umeme vijijini kupita REA Awamu ya Tatu.
Aliongeza kuwa kupitia REA Awamu ya Pili wakandarasi wa kitanzania
walionyesha uwezo mkubwa sana katika kusambaza umeme vijijini.
Ili
kuendana na mahitaji ya umeme nchini Profesa Muhongo alilitaka Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linaongeza Megawati 200 za ziada
ndani ya miezi 18.
Alisema
wakati serikali kupitia REA ikiendela na kasi yake ya kusambaza umeme
nchi nzima, shirika la TANESCO linatakiwa kuhakikisha nishati ya uhakika
inapatikana ikiwa ni pamoja na ubunifu wa vyanzo vipya vya umeme.
Awali
akielezea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga, Meneja
wa Shirika la Umeme Tanzania mkoani Tanga, Mhandisi Abdulrahman Nyenye
alisema kuwa miradi ya umeme vijijini chini ya ufadhili wa REA imekuwa
ikitekelezwa katika wilaya zote nane za mkoa wa Tanga ambazo ni pamoja
na Tanga Mjini, Muheza, Korogwe, Handeni, Kilindi, Lushoto, Pangani na
Mkinga ambazo zinapata umeme wake kutoka Gridi ya Taifa kupitia vituo
vya Hale, Kange na Tanga (Majani Mapana)
Alisema
kundi la kwanza lilihusisha wilaya za Korogwe, Lushoto, Handeni na
Kilindi ambapo mradi wa wilaya hizi ulitekelezwa na mkandarasi STEG
International Services Ltd ya Tunisia na kusimamiwa na TANESCO.
Alifafanua
kuwa gharama za mradi huo ilikuwa ni Dola za Marekani 9,463,502 ambazo
ni sawa na shilingi bilioni 14.6 na kuendelea kusema kuwa kundi la pili
lilihusisha wilaya za Muheza, Mkinga, Tanga Vijijini na Pangani na
kutekelezwa na mkandarasi Sengerema Engineering Group Ltd ya Tanzania na
kusimamiwa na TANESCO.
Alisema
kuwa mradi huu uligharimu shilingi bilioni 15.6 na kusisitiza kuwa
miradi yote kwa mkoa wa Tanga imekamilika kwa asilimia 99 ambapo jumla
ya vijiji 178 vimepatiwa huduma ya umeme.
Akielezea
changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo Mhandisi Nyenye alieleza
kuwa ni pamoja na tatizo la wananchi kuzuia upitishwaji wa laini za
umeme kwenye maeneo yao kwa kudai fidia ili kuruhusu mazao yao yakatwe
na hali ya hewa ya mvua isiyotabirika hasa maeneo ya wilaya za Muheza na
Lushoto.
Alitaja
chagamoto nyingine kuwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu hasa ya
barabara kwenye maeneo mengi , hali duni ya kiuchumi ya wananchi
inayopelekea wananchi kushindwa kulipa gharama za kuunganishiwa umeme na
gharama kubwa za ukaguzi wa miundombinu ya ndani (wiring) zinazotozwa
na wakandarasi ambazo zimekuwa ni kikwazo kwa wananchi wanaohitaji
huduma ya umeme.
EmoticonEmoticon